Nenda kwa yaliyomo

Klara wa Asizi

Kutoka Wikibooks

KLARA WA ASIZI

Mt. Klara, aliyejiita “mche mdogo wa Mt. Fransisko”, ndiye jiwe la msingi la Utawa II ulioleta karama ileile ya Ndugu Wadogo kwa wanawake na kwa kujifungia faraghani. Ndizo nguzo mbili za utawa huo.

Binti huyo wa ukoo bora alizaliwa Asizi (1193). Kisha kuvutiwa na mifano ya Mt. Fransisko, na kusikiliza mahubiri na mashauri yake, akaamua kujiweka wakfu kwa Kristo katika ufukara mkuu. Basi, akatoroka nyumbani usiku (1212) akamuendea Mt. Fransisko huko Porsyunkula ambapo alinyolewa naye na kuvikwa kanzu, kamba na shela nyeusi. Kesho yake asubuhi akapelekwa kwa masista Wabenedikto, na baada ya wiki mbili kwenye monasteri yao nyingine, alipofikiwa na mdogo wake (Mt. Anyesi) ambaye pia alipaswa kukabili upinzani mkali wa ukoo wao. Mt. Fransisko alipomaliza kuandaa jengo la Mt. Damiano, wakahamia huko kushika maisha ya ndani, wakaongezeka haraka. Miaka 40 baadaye Mt. Klara akaja kuandika kwamba mwanzo ulikuwa mgumu na walidharauliwa sana. Mwaka huohuo (au ule uliofuata) mwanzilishi, alipoona walivyovumilia yote, aliwaandikia kwa ufupi “mtindo wa maisha”. Wakati huo aliwaomba wamsaidie kutambua kama Mungu anataka yeye na Ndugu Wadogo waishi upwekeni tu au wafanye utume pia. Jibu likawa kwamba wakahubiri; lakini Mt. Klara na wenzake watawafuata kiroho tu kwa sala na sadaka, wakichangia urekebisho wa Kanisa bila ya kutoka nje ya kiota chao.

Baada ya Mtaguso IV wa Laterano (1215) kukataza kanuni mpya iliwabidi wapokee mojawapo ya zamani ili wakubaliwe na Kanisa kama watawa. Basi wakaichagua ile ya Mt. Benedikto, wakiifuata katika mambo kadhaa kadiri yalivyopatana na mtindo wao mpya, bila ya nia ya kuwa Wabenedikto. Hapo ilimpasa Mt. Klara kuitwa abesi, jina alilolikubali tu kwa kumtii mwanzilishi, ingawa akaendelea kujiita “mtumishi wa Kristo na wa akina dada fukara”. Hasa Mt. Klara hakutosheka na uhalali wa monasteri yake mbele ya Kanisa, bali kwa njia ya Mt.Fransisko aliomba akapewa na Inosenti III “fadhili ya ufukara” (1216), yaani ruhusa ya kuishi bila ya mali hata kijumuia, kama jambo la msingi katika wito wake wa “kuishi kadiri ya ukamilifu wa Injili takatifu”, kwa kuungana na Kristo fukara kama bibiarusi fukara.

Kardinali Ugolino, akiona monasteri za namna hiyo zinavyoongezeka huko na huko, alizitungia katiba (1219) iliyopitishwa na Honori III (1216-1227) ambayo ikawa msingi wa kanuni zote zilizoandikwa baadaye kwa Utawa II. Lengo lake lilikuwa kukinga monasteri hizo dhidi ya upinzani na kuzipa mtindo wa kimonaki zaidi bila ya kuondoa usahili wake maalumu, ziwe muundo mpya wa aina moja chini ya Kanisa la Roma moja kwa moja. Katika juhudi zake za kurekebisha umonaki alielekeza hata monasteri kadhaa za zamani zifuate mtindo wa Mt. Damiano. Desturi kali alizoziagiza humo hazikumtisha Mt. Klara, ambaye alijishinda tayari na kujitesa kwa ushujaa mkubwa (katika kula, kuvaa, kulala n.k.) mpaka akakatazwa asizidishe. Wala hakuogopa ukali wa ugo ulioagiwa na katiba hiyo, ili kutunza mazingira ya sala. Wasiwasi wake ulihusu ufukara mkuu akiona hautajwi na katiba hiyo. Mwanzoni Ugolino alitaka msimamo huo udumu katika monasteri kadhaa, ila alipochaguliwa kuwa Papa akaanza kuzipatia mali nyinginyingi, labda kisha kung’amua matatizo yaliyojitokeza. Lakini Mt. Klara hakukubali kabisa akamuomba amtibitishie “fadhili ya ufukara” akakubaliwa (1228), lakini si kwa monasteri zote.

Suala lingine lililojitokeza mapema, halafu likaendelea kusababisha migogoro, ni nani awajibike kuwasaidia Waklara upande wa roho na upande wa riziki. Mt. Fransisko alipokuwa Mashariki, nd. Filipo Longo aliteuliwa msimamizi wao, lakini mwanzilishi aliporudi uteuzi huo ukafutwa, masista wakasimamiwa tena na wasio Wafransisko, mpaka Gregori IX alipowalazimisha Ndugu Wadogo kuwajibika (1221).

Mt. Klara alipoona wito wake wa Kiinjili upo hatarini upande wa sheria, kwa kuwa kanuni na katiba hazikuwa za Kifransisko, akaanza kuomba aweze kuahidi kushika kanuni ya Ndugu Wadogo badala ya ile ya Mt. Benedikto. Mwaka 1234 akaja kumuunga mkono Mt. Agnesi wa Praha, binti mfalme ambaye alikataa kuolewa na mfalme mkuu Federiko II wa Ujerumani akaanzisha monasteri yake iliyokubaliwa “fadhili ya ufukara”. Alitunga kanuni mpya kwa kuchanganya “mtindo wa maisha” alioandika Mt. Fransisko na katiba ya Ugolino, akamuomba Gregori IX, halafu Inosenti IV waithibitishe, lakini akakataliwa. Kumbe Inosenti IV akathibitisha katiba ya Ugolino (1245) na kusisitiza ifuatwe kanuni ya Mt. Benedikto kwa sababu ina sifa nyingi. Wakati huohuo alijaribu kusuluhisha mgogoro wa uhusiano kati ya Ndugu Wadogo na Waklara. Mt. Klara alikuwa akiendelea kudai kwa nguvu msaada wa kiroho wa ndugu hao kulingana na ahadi ya mwanzilishi. Kumbe Mtumishi mkuu Kreshensi wa Iesi aliomba shirika liondolewe mzigo liliobebeshwa na Gregori IX, yaani himizo la kuanzisha konventi ndogo karibu na kila monasteri ya Waklara. Basi, Inosenti IV aliamua Waklara wawe chini ya uongozi na mamlaka ya Ndugu Wadogo, akapendekeza masista waunganishwe na Utawa I. Lakini shirika likazidi kuona litalemewa na wingi wa monasteri.

Mwaka 1247 Inosenti IV akatunga katiba mpya badala ya ile ya Ugolino iliyokwishaenea katika monasteri zote za Kifransisko, ikitumika pengine pamoja na desturi maalumu za mahali. Katiba hiyo ilifanya kanuni ya Ndugu Wadogo kuwa msingi wa sheria za Waklara bila ya kuwadai waishike katika yote, ila katika utiifu, utovu wa mali na useja mtakatifu. Katiba hiyo ilimuondolea Kardinali mlinzi mamlaka juu ya Waklara, ambao wakawekwa moja kwa moja chini ya viongozi wa Utawa I. Kwa katiba hiyo Waklara wakaja kutambulikana Wafransisko kisheria, lakini ndani mlikuwa na pigo kubwa kwa Mt. Klara, yaani iliandikwa wazi kuwa monasteri zao zinaruhusiwa kuwa na mali za kujitegemea. Ndiyo sababu monasteri chache tu zikaipokea katiba hiyo. Vilevile Ndugu Wadogo wakazidi kulalamika hadi Kardinali mlinzi akajitwalia polepole mamlaka yao na hatimaye (1250) aliwaandikia wasithubutu kujiingiza katika uongozi wa Waklara. Hivyo kwa muda mfupi katiba hiyo ikashindikana pande zote.

Mt. Klara, mgonjwa toka siku nyingi, alipoona kifo kinamkaribia, aliandika wasia wake ambamo alimuiga Mt. Fransisko katika kukumbusha asili ya wito wake na wa jamaa yake, na kutamka kwa msisitizo mkubwa nia imara ya kufuata ufukara mkuu “aliouahidi kwa Mungu na kwa Mt. Fransisko” pamoja na kuhimiza sana umoja wa dada zake. Lakini pia, upande wa sheria, aliona haja ya kutunga upya “mtindo wa maisha” kwa kulinganisha kanuni ya Ndugu Wadogo na masharti ya maisha ya ndani tu. Humo aliingiza pia maandishi mawili mafupi ya Mt. Fransisko kwao, kuhusu ufukara mkuu na kuhusu ahadi ya kwamba yeye na Ndugu Wadogo watawahudumia Waklara sawa na wenzao wa kiume. Upande wake Mt. Klara aliahidi kuwatii waandamizi wa mwanzilishi. Kiini cha huo “mtindo wa maisha” kinasisitiza kwa nguvu nia ya kuishi bila ya mali yoyote, isipokuwa monasteri na bustani. Jambo lingine linalokazwa ni udugu: humo neno “dada” linapatikana mara 66! Udugu huo unatimizwa siku kwa siku chini ya “abesi na mama” kwa umoja wa mioyo pasipo ubaguzi wowote (tofauti pekee ni kati ya wanaojua na wasiojua kusoma kuhusu Sala ya Kanisa). Hata dada “wa nje” (yaani “wanaohudumia nje ya monasteri” bila ya kubanwa na ugo) washiriki maisha ya jumuia sawa na wenzao. Hao ni kundi maalumu la mtindo wa Kiklara, linalohitajika kadiri wenzao wanavyojifungia ndani: ni “akina Marta” kwa “akina Maria” kadiri Mt. Fransisko alivyowapangia Ndugu Wadogo wanaoishi upwekeni. Udugu huo unajitokeza hata katika mikutano, ambayo inatakiwa kufanyika kila wiki kwa mchango wa wote, kupanga shughuli za maana na kuteua watakaoshika nyadhifa mbalimbali. Abesi mwenyewe, ingawa anachaguliwa kwa maisha yake yote, kadiri ya mapokeo ya kimonaki, anaweza kubadilishwa dada zake wakiona hawezi kutimiza vizuri kazi zake. Uhusiano na Utawa I unasisitizwa tena kwa kudai msimamizi wa monasteri awe daima Ndugu Mdogo, pamoja na kuomba Utawa huo uipatie monasteri mapadri 2 na mabradha 2 kwa huduma za kiroho na za kimwili.

Huo “mtindo wa maisha” ukakubaliwa na Kardinali mlinzi (1252) halafu na Inosenti IV (1253). Mt. Klara akapewa hati yake kitandani akaibusu; siku mbili baadaye akafa akiishika mikononi, wakihudhuria nd. Leo, nd. Angelo na nd. Ginepro wenzi wa Mt. Fransisko; pia alijaliwa faraja za Bikira Maria na wanawake watakatifu kadhaa. Mazishi yalihudhuriwa na Papa, Makardinali, Maaskofu na wengineo. Inosenti IV alitaka ziimbwe sala za watakatifu mabikira badala ya zile za wafu, ila akakubali shauri la Kardinali mlinzi la kufuata taratibu zilizopangwa kabla mtu hajatangazwa mtakatifu. Miaka miwili baadaye, Kardinali huyo akiwa amepewa Upapa kwa jina la Aleksanda IV (1245-1261), akamtangaza rasmi kuwa mtakatifu (1255). Mwaka 1260 masalia yake yakahamishiwa mjini Asizi katika kanisa lililojengwa kwa heshima yake.

Pamoja na kanuni na wasia, Mt. Klara ametuachia walau barua nne (kwa Mt. Agnes wa Praha). Maandishi hayo ndiyo chemchemi ya kwanza ambamo tuchote utajiri wa roho yake na wa utu wake. Hasa ya mwisho inatuonyesha alivyogeuka ndani ya Yesu kwa kuzidi kumkazia macho kama kioo chake na kujifunza toka kwake hasa ufukara, unyenyekevu na upendo wa ajabu, vilivyong’aa katika hatua mbalimbali za maisha yake kuanzia Bethlehemu hadi Kalivari. Mt. Klara alimfikia Mungu kwa kumfuata Yesu kama bibiarusi mwaminifu katika hatua hizo za maisha yake halisi, kama alivyoelekezwa na Mt. Fransisko, kadiri ya karama yake mpya katika kumtazama Yesu na kuelewa Injili.