Sala ya Moyo

Kutoka Wikibooks
Jump to navigation Jump to search

SALA YA MOYO

Sala ya moyo ni aina ya sala inayofanywa na mtu peke yake, hata bila ya kutamka maneno kwa sauti. Hapa tutaieleza kadiri ya mapokeo ya Kikristo.1. SALA YA MOYO SI…

Kwanza tuondoe au kusahihisha baadhi ya mawazo yaliyoenea sana kuhusu kazi hiyo bora.


1.1. SALA YA MOYO SI KUTAFAKARI TU


    Sala ya moyo si kupanga mawazo tu, hata kama ni mawazo mazuri ya dini. Katika sala ni lazima akili itumike, lakini haitoshi mpaka niseme na Mungu. Hasa mawazo yanatakiwa kuwasha moto wa upendo ndani mwangu. 


1.2. SALA YA MOYO SI KUJISOMEA TU


    Sala ya moyo si kujisomea tu, hata kama ni vitabu vizuri vya dini. Kitabu, na hasa Biblia, kinaweza kikasaidia kufukuza mawazo mengine na kuingiza katika mafumbo, lakini hakitoshi mpaka nianze kusema na Mungu. 


1.3. SALA YA MOYO SI KUSEMA TU


    Sala ya moyo si kusema tu, karibu mfululizo, hata kumnyima Mungu nafasi yake. Sitakiwi kukusudia ninyamaze kabisa mbele yake, lakini pia nisiseme peke yangu. Kama vile ninavyomuambia kimoyomoyo maneno yangu, niwe tayari kusikiliza moyoni maneno yake pia. 


1.4. SALA YA MOYO SI KUFUATA RATIBA TU


    Sala ya moyo si kufuata ratiba tu, ingawa hiyo inanisaidia nisije nikasahau wala kulegea katika kuongea na Mungu. Tunaweza kupanga kijumuia saa ya sala ya moyo, lakini kila mmoja atasali peke yake na kwa namna yake, tofauti na liturujia ambayo ni sala ya Kanisa zima. Nisiende kusali kwa kuwafuata wenzangu, bali kwa kumfuata mpenzi wangu. 


1.5. SALA YA MOYO SI KUFANYA ZOEZI TU


    Sala ya moyo si kufanya zoezi tu, hata kama ni la kutulia na kujikusanya, mpaka nianze kusema na Mungu. Kwa kuwa lengo la zoezi la namna hiyo ni kwamba nizame ndani yake na kuungana naye kwa upendo. 


1.6. SALA YA MOYO SI KUJIKAZA TU


    Sala ya moyo si kujikaza tu, hata kama ni kwa lengo la kutawala mawazo yangu. Nikitaka kuongea na Mungu ni lazima nifanye bidii, lakini si mpaka niumwe kichwa au kujichosha kabisa. Niwe na utulivu wa roho kwa kuwa namkaribia mpenzi wangu. 


1.7. SALA YA MOYO SI KAZI YANGU BINADAMU TU


    Sala ya moyo si kazi yangu binadamu tu, ingawa natakiwa kuichangia kwa juhudi. Zaidi napaswa kumtegemea Roho Mtakatifu ambaye yumo ndani mwangu na anataka kusali kwa njia yangu. 


1.8. SALA YA MOYO SI KUFARIJIKA TU


    Sala ya moyo si kufarijika tu, ingawa Mungu kwa wema wake anaweza akatufariji kwa utamu wake. Lakini nikubali afanye hivyo anapotaka yeye akiona ni vizuri kwangu. Nikipata faraja nimshukuru; nisipopata niendelee kusali, la sivyo nitaonyesha kuwa napenda faraja zake kuliko ninavyompenda mwenyewe. “Nzi anayetaka kuonja utamu wa asali akizamisha mabawa yake ndani ya asali hawezi kuruka tena. Vivyo hivyo mtu anayetaka kufurahia matamu ya roho hawezi kuinukia sala hasa” (mt. Yohane wa Msalaba). 


1.9. SALA YA MOYO SI KUSAHAU MAISHA NA WAJIBU


    Sala ya moyo si kusahau maisha na wajibu, ili kusema na Mungu juu ya mambo ya dini tu. Nikitaka kuongea naye ni lazima nizuie mawazo yangu yasitawanyike ovyo hata nikamsahau, lakini naweza kumuendea pamoja na maisha yangu yote, hasa wito, wajibu, matatizo, furaha niliyo nayo n.k. Muhimu ni kwamba niongee naye kuhusu mambo hayo ili niyaone upya kwa mwanga wake. 2. SALA YA MOYO NI…

“Sala ya moyo ni uhusiano wa dhati wa kirafiki ambao mtu anawasiliana na Mungu moja kwa moja, akijua kwamba anapendwa naye, na akiwa na lengo la kuishi vizuri zaidi ndani mwake” (mt. Teresa wa Yesu).


2.1. SALA YA MOYO NI KUTULIA MBELE YA MUNGU


    Ninapokwenda kusali kwa moyo naacha shughuli na kusimama kidogo ili niongee na Mungu na kumtolea maisha yangu yote yazidi kumpendeza kama yale ya Mwanae. Nimshirikishe yote ya kwangu kwa kuwa mwenyewe anataka kuhusika nayo na kunitengeneza upya kwa upendo. Naweza kuhusiana naye kazini au njiani pia, lakini hasa kama nimezoea kufanya hivyo katika sala, nikizingatia kwamba yumo kweli ndani mwangu hata niweze kumjua na kumpenda kwa furaha. 


2.2. SALA YA MOYO NI KUONGEA NA MUNGU


    “Si lazima tuinuke mpaka mbinguni ili kuongea na Mungu, wala hatuhitaji kupiga kelele ili atusikilize. Mungu yupo karibu nasi hata asikie minong’ono ya midomo yetu, hata maneno ya moyoni. Hatuhitaji mabawa tukamtafute. Tufunge kidogo mlango wa nje, tukae peke yetu na kujitazama ndani: yeye yumo humohumo” (mt. Teresa wa Yesu). Lengo la sala hiyo ni “kuongea moyo kwa moyo” (mt. Teresa wa Yesu). Yesu alimuambia mh. Angela wa Foligno: “Kama mtu akitaka kunipata rohoni mwake sitamkatalia. Kama mtu akitaka kuniona nitamjalia kwa moyo aone uso wangu. Kama mtu akitaka kusema nami tutaongea pamoja kwa furaha kubwa ajabu”. 


2.2.1. MAONGEZI YA MACHO


    Tusisahau jibu la mkulima wa Ars alipoulizwa anasali vipi: “Sisemi kitu ili namtazama, naye ananitazama”. Charles de Foucald alifafanua kuwa sala ya moyo ni hali ambayo mtu anamtazama Mungu bila ya maneno, naye kwa macho tu anamuambia kuwa anampenda, ingawa midomo, na pengine hata akili imenyamaza. Si kwamba anatumia macho ya mwili, bali ya roho. Sala bora ni ile ambayo macho hayo yamejaa upendo mkubwa zaidi. 


2.2.2. MAONGEZI YA MIOYO


    Mt. Teresa wa Mtoto Yesu aliulizwa anamuambia nini Mungu akajibu, “Simuambii kitu chochote, ila nampenda tu”. Basi, nikitaka kuwaka moto wa upendo kwake, nizingatie alivyonipenda upeo katika kuniumba, kujifanya mtu, kuteseka na kuniita mbinguni ili nipendane naye milele. Hata leo ananipenda jinsi nilivyo, pamoja na kasoro zangu, na kwa upendo huo anataka kunifanya mtakatifu. Kazi yangu ni kukubali nipendwe hivyo na kumrudishia upendo hata bila ya maneno. Kwa kuwa upendo wake unanidai upendo, tena upendo wake ndio unaozaa upendo wangu. 


2.2.3. MAONGEZI YA UTASHI


    Anayependa anataka kumpendeza mpenzi wake katika yote. Basi, nimuulize Bwana anataka nifanye nini, halafu nimueleze nataka anifanyie nini, nikijiombea, pamoja na neema nyingine, ile ya kusali vizuri. 


2.3. SALA YA MOYO NI KUBADILISHANA NA MUNGU


Hali ya sala iliyojaa imani, tumaini na hasa upendo inafanya niweze kubadilishana na Mungu kiburi changu na unyenyekevu wake, ubinafsi wangu na upendo wake, unyonge wangu na ukuu wake, udhaifu wangu na uwezo wake.
3. SABABU ZA KUSALI KWA MOYO

Ni muhimu nijue sababu za kusali kwa moyo niweze kuwa imara katika bidii hiyo ya lazima.


3.1. KWA AJILI YA MUNGU


3.1.1. MUNGU ANANINGOJEA


Ninapokwenda kusali niwe na hakika ya kuwa Mungu atanipokea, tena ananingojea kwa hamu kubwa. Hamu yake ndiyo iliyosababisha niamue kumuendea.


3.1.2. MUNGU ANA HAKI HIYO


Tangu zamani Mungu aliwadai Waisraeli wamtolee siku moja kwa wiki na sehemu moja ya kumi ya mali alizowajalia. Ndiyo alama ya shukrani na ya imani kuwa ndiye Bwana na asili ya mema yote, hasa ya uzima wetu. Pamoja na hayo Mungu ni mkarimu kuliko wote na anatuzidishia baraka kwa yale yote tunayomrudishia.


3.2. KWA AJILI YANGU MIMI


3.2.1. SALA YA MOYO INANIJAZA NEEMA


Mungu ni mkarimu kwa sababu ni upendo: hivyo anapenda kujitolea hata kujitoa na kushirikisha umungu wake. Katika sala ya moyo najiweka mbele yake katika ukweli nikiwa tayari kupokea neema zake.


3.2.2. SALA YA MOYO INANITIA MWANGA NA NGUVU YA MUNGU


Mungu ananipatia neema kadiri ya hamu yangu ya kuzipata. Katika sala ya moyo ni wazi kwamba nataka kumfahamu na kumpenda, kumtii na kujaliwa kwa wingi. Basi, Mungu anakuja kunijaza neema hizo hata zinaonekana katika maisha yangu na kazi zangu. Nikijitahidi kushirikiana na Roho Mtakatifu katika sala mwanga wake utaenea katika mawazo na maneno yangu. Hivyo, bila ya kutegemea, nitaelewa neno fulani la Biblia au tukio fulani la maisha yangu; pia nikisema neno katika utume litakuwa na nguvu ya kuigusa mioyo ya watu.3.2.3. SALA YA MOYO INANIZIDISHIA IMANI, TUMAINI NA UPENDO


Maadili hayo makuu siwezi kujipatia, bali najaliwa na Mungu hasa kwa njia ya sala. Lakini kwa kuwa maadili ni mazoea ya kutenda mema, natakiwa kurudiarudia matendo yake. Basi, katika sala ya moyo natumia sana imani, tumaini na upendo nikizingatia mambo makuu kuliko maisha ya kila siku, pamoja na kutazama yote kwa mwanga wake. Mwanga huo hauishii juujuu, bali unanionyesha ukweli wa mambo mpaka ndani, hata ubora wa mateso na misalaba ya maisha yangu. Hivyo imani inakua ikichanua tumaini na kuzaa upendo. Tumaini linakua hasa katika mambo matatu: kutamani ufalme wa Mungu, kutegemea ulinzi wake, kumkabidhi aongoze maisha yangu. Hivyo upendo pia unakua kwa kutaka zaidi nilingane na matakwa yake.


3.2.4. SALA YA MOYO INAIMARISHA MAISHA YANGU YA KIROHO


Tofauti na wanyama, mimi kama binadamu natakiwa kuishi sio kimwili tu, bali hasa kiroho: yaani sio tu kwa ajili ya kula na kunywa, kuzaa na kustarehe, bali hasa kwa kushirikiana na Mungu na pia na watu, kwa njia ya upendo. Hivyo sitakiwi kuzingatia tu vitu vinavyoonekana, bali hasa mambo yasiyoonekana. Naweza kuyazingatia hata wakati ninapotimiza haja za mwili, lakini si rahisi kufanya hivyo kama sijazoea sala ya moyo. Bidii katika sala hiyo itafanya niishi kiroho saa zote kwa kuwa naja kuzoea kufikiri na kuelewa ukweli wa mambo, nikiongozwa na Roho Mtakatifu. Nitafanya hivyo katika matendo yangu pia, badala ya kufuata tu maelekeo yangu na tamaa mbalimbali.


3.2.5. SALA YA MOYO INANITAKASA


Nimeathiriwa na vilema mbalimbali, kiasi kwamba matendo mema pia yamejaa umimi, kiburi, majivuno n.k. Katika sala naja kuvitambua hivyo vyote. Nikiona matukio madogomadogo yananiathiri au kunikasirisha au kunikatisha tamaa, nijue kwamba nahitaji kutulia zaidi katika sala ya moyo. Kwa kumtazama Mungu, Yesu na Maria, kwa kufikiria maneno yao, kwa kutamani nilingane nao, na kwa kutafakari ubaya wa dhambi, nitajielewa na kuimarishwa. Hivyo nitazidi kuelewa udogo wangu na kukubali kwa unyenyekevu nishike nafasi yangu katika mpango wa Mungu.


3.2.6. SALA YA MOYO INAMSHINDA SHETANI


Shetani anajua fika faida ninayopata kwa sala yangu, hasa ile ya moyo. Basi, anajaribu kwa kila namna kunikatisha tamaa nisisali. Ndiyo sababu Yesu kwa maneno na mifano ya maisha yake alisisitiza lazima ya kukesha na kusali. Kwa kushindwa sala ya moyo bustanini, mitume wake wakaja kumkimbia na hata kumkana. Nikiyajua hayo, nikazanie sala ya moyo: hapo matendo yangu yote yatakuwa na uhai, kwa kuwa Mungu atakuwa nami.


3.3. KWA AJILI YA WENZANGU


Nimeitwa na kutumwa hasa kwa kipaimara nimshuhudie Yesu mwema kwa maneno na matendo yangu ya kila siku. Watu ambao hawamjui wala hawamtafuti wanaweza kukutana naye kwa njia yangu, mradi niwe kweli mtu wa Mungu na si msemaji tu. Natakiwa kufanya sala ya moyo kwa bidii pia kusudi niwe mtu wa namna hiyo na kuwasaidia wenzangu. Nisipojifunza mwenyewe, nitawezaje kuwafundisha wengine? Siwezi kutoa kile nisichonacho.4. MAANDALIZI YA SALA YA MOYO

Ninapokwenda kusali kwa moyo kitu cha lazima zaidi ni kutaka kumkaribia Mungu: hiyo iwe ndiyo hamu au kiu ya roho yangu. Itakuwa rahisi zaidi kumkaribia hivyo nikizidisha sala na sadaka ndogondogo za saa zote. Hasa nimkaribie kwa unyenyekevu, nikikumbuka unyonge wangu na ukuu wake.


4.1. KUCHAGUA MUDA WA KUSALI


Sala ya moyo inaweza kufanyika saa yoyote, asubuhi, mchana, jioni au usiku. Lakini kila mtu ana muda fulani unaomfaa zaidi kwa kukusanya mawazo na kusali. Basi, nikiwa peke yangu nijichagulie muda huo. Katika jumuia inafaa kupanga nafasi mbalimbali ili wote wafaidike.


4.2. KUPANGA UREFU WA SALA


Kila mtu anaweza kujipangia au kupangiwa na kiongozi wa kiroho urefu wa sala ya moyo kulingana na hali yake, shughuli zake na maendeleo yake. Lakini muhimu zaidi ni kutekeleza mpango huo bila ya kupunguza muda wa sala wala kulegeza bidii muda huo wote, la sivyo anayesali dakika tano tu anaweza akafaidika kuliko anayesali saa nzima. Pamoja na hayo, nijue kwamba mara nyingi dakika za mwisho zina neema za pekee, na kwamba nikijiongezea kwa hiari dakika moja au mbili Mungu atanilipa kwa ukarimu.


4.3. KUCHAGUA MAHALI


Sala inafanyika moyoni: ndimo ninapokutana na Mungu wangu. Hata hivyo mahali pana umuhimu wake katika kusaidia au kuzuia sala yangu. Kila mtu ana mahali ambapo anafaulu zaidi, k.mf. msituni au mlimani au chumbani. Kwa walio wengi sala inakuwa rahisi kanisani, hasa penye tabenakulo. Baadhi wana kipaji cha kusali vizuri hata penye kelele. Basi, ninapoweza kujipangia mahali nichague panaponifaa zaidi, bila ya kujidanganya.


4.4. KUCHAGUA NAMNA YA KUKAA


Ingawa sala ni ya moyo, namna ya kukaa kwa mwili inaweza kusaidia. Kila mtu ana namna yake, lakini kwa kawaida zile za kujitesa au kujipumzisha mno zinazuia sala.


4.5. KUCHAGUA LA KUONGEA


Naweza kuongea na Mungu kuhusu lo lote lakini ni vizuri niandae la kuwaza na kusema, nisije nikapoteza muda. Nikitaka kutumia kitabu nisisahau kwamba kusoma ni kama kuongea na mwandishi, kumbe lengo langu ni kuongea na Mungu. Kitabu ni msaada tu, ni kama kiberiti cha kuwashia moto wa sala. Kwa hiyo niwahi kukiacha nikiona niko karibu naye kwa imani, tumaini na upendo.

Huenda nikapata ghafla wazo tofauti ambalo linanivutia: basi, nipokee neema hiyo kwa mikono miwili, kwa kuwa ni Mungu anayenipangia maongezi naye. Niendelee na wazo hilo nikijua kwamba ameniandalia neema zake kwa njia hiyo. Vivyo hivyo, nikiwa na maombi, niyatoe, mradi niweke mbele mapenzi yake.


4.6. MAANDALIZI YA KUDUMU


Baada ya kuzingatia hayo yote tunayoweza kuyaita maandalizi ya mara moja, nikumbuke kuwa ni muhimu zaidi maandalizi ya kudumu, yaani bidii ya kila saa ya kukwepa dhambi yoyote na kutenda mema mengi. Nikilegea katika maadili, sala itaathirika mara, kwa sababu kuna ulinganifu mkubwa wa sala na maisha yangu. Sala inanipatia nguvu ya kuishi vema, na maisha mema yananiandaa nisali vema.


4.6.1. UNYENYEKEVU


“Sala ya mnyenyekevu hupenya mawingu”. Nijitahidi kila siku kupata unyenyekevu na kuwa na moyo kama wa mtoto mdogo au wa mtu fukara au wa mkosefu aliyetubu. Hivyo kila nitakapokwenda kusali nitafanikiwa. “Mungu anapotaka kuifadhili roho ya mtu, hatazami ukuu wake bali ukweli wa ndani wa unyenyekevu wake na jinsi anavyojidharau” (mt. Yohane wa Msalaba).


4.6.2. MOYO WA SADAKA


Katika sala nataka kukutana na yule aliyejishusha na kuteseka kwa upendo wangu. Basi ni lazima nifuate njia hiyohiyo kwa kumtolea Mungu sadaka ya vitu mbalimbali. Kila ninapojikatalia kwa ajili yake imani inakua. Katika anasa siwezi kusali kweli.


4.6.3. UPENDO


Mungu ni upendo, na sala ya moyo ni sala ya upendo. Lakini nikumbuke daima kuwa upendo kwa Mungu na kwa jirani ni mmoja tu. Kwa hiyo sala inanidai nizidishe matendo ya upendo kwa wenzangu, na hasa niondoe chuki, kinyongo, dharau n.k.


4.6.4. ROHO YA SALA


Sala ya moyo inatakiwa kuwa kilele cha kazi ya saa zote, yaani kumfikiria Mungu hata katika shughuli za kawaida. Nikimsahau wakati huo na kutawanya mawazo ovyo, hata katika sala ya moyo itakuwa vigumu kumkumbuka. Upande mwingine, sala ya moyo inanizoesha kumkumbuka Mungu na hivyo inakuwa rahisi kuwa naye hata katika kazi.


4.6.5. MOYO WA IBADA KWA ROHO MTAKATIFU NA KWA BIKIRA MARIA


Shauri la mwisho ni kuwapenda na kuwaheshimu Roho Mtakatifu na Bikira Maria. Roho Mtakatifu ndiye msaidizi mkuu katika sala. Bikira Maria ni kielelezo cha kupokea neema za Mungu. Hivyo kadiri nitakavyowaheshimu, sala itakuwa rahisi. Inafaa niongee nao hasa mwanzoni mwa sala ya moyo ili waniongoze.5. UTEKELEZAJI WA SALA YA MOYO

    Baada ya kujitayarisha, nifanye nini? 


5.1. KUMTAZAMA MUNGU


    Mambo muhimu zaidi ninaposali kwa moyo ni kumtazama Mungu kwa upendo ili kumsikiliza nikiwa tayari kutii. Nimtazame kwanza kwa macho ya imani, kama anavyofanya mtu anayemtazama mpenzi wake macho wazi kwa upendo mwingi. Nisianze kusema lolote nisipotambua kwa imani kwamba namuelekea kweli Mungu hata niweze kumuambia kwa unyofu: wewe hapa. 


5.2. KUANZA MAONGEZI


Baada ya kumpata mwenzangu huyo niongee naye kwa kusema lakini hasa kwa kusikiliza. Kama kawaida ya maongezi yoyote, yanaweza kuanza na kuendelea vizuri ikiwa pande zote mbili zinachangia; lakini yanafanyika kwa shida ikiwa mmoja au wote wawili hawashiriki vizuri katika kusema na kusikiliza. Upande wangu niwe tayari kumsikiliza na kumuitikia Mungu akipenda kuanza mwenyewe; vilevile niwe tayari kuanza mimi na neno fulani (k.mf. kutoka Biblia au liturujia au matukio) nikiona amenyamaza.

Kusema niseme kwa moyo hata nikitumia sala za mwingine: kama maneno yake hayalingani na moyo wangu itakuwa kazi bure. Kadiri ya hali yangu, sala inaweza kuingia upande wa shukrani au sifa au tumaini au majuto au ombolezo au mengineyo, mradi nimuelekee kweli Mungu na kusema naye.

Kusikiliza nimsikilize Mungu hasa katika Biblia: ni mawazo yake, ni maneno yake, ni maandishi yake kwa ajili yangu pia. Alipoiandikisha alijua ataitumia vipi hapo baadaye katika kuongea na watu, alijua kwamba mimi pia nitakuja kuisoma akapanga ataniangaza kwa maneno gani leo na kesho. “Kabla ya yote katika kutafakari kwangu natumia Injili: ndani yake naona yale yote ambayo roho yangu maskini ndogo inayahitaji. Ndani yake naona daima mwanga mpya na maana zilizofichika na za kifumbo… Naelewa, tena najua mwenyewe ya kuwa ufalme wa Mungu umo ndani mwetu. Yesu katika kuzifundisha roho zetu hahitaji vitabu wala walimu: yeye ni dokta anayefundisha bila ya kelele ya maneno… Sijawahi kumsikiliza akisema, lakini nasikia kuwa yumo ndani mwangu. Kila dakika ananiongoza, naye ananitia moyoni niseme nini kwa Baba. Palepale ninapohitaji naona mianga ile ambayo nina shida nayo na ambayo sijaiona” (mt. Teresa wa Mtoto Yesu).

Nikiona kiberiti kimewasha nisiendelee kusoma, bali nizingatie maneno yaliyoniangaza kwa kuyarudiarudia moyoni mwangu au hata kwa sauti ndogo. Muhimu ni kuamini kwamba ninaambiwa hayo na Mungu, au kumuambia hayohayo pengine kwa kubadilisha sentensi imuelekee yeye. Kazi hiyo ni kama kuonja na kufurahia utamu wa kinywaji au kukamua majamaji yote ya chungwa. Ikiwa punde baadaye maneno hayo hayanivutii tena, naweza kushika tena kitabu na kurudia kusoma palepale au kwenda mbele kidogo. Naweza pia kumshirikisha Bikira Maria anisaidie kutafakari maneno hayo kama alivyokuwa akifanya mwenyewe kuhusu maneno ya Yesu.


5.3. KUTUMIA VIPAWA VYANGU


Kusudi nisikate tamaa nikiona mawazo yanaendelea kutawanyika, niwe na hakika ya kuwa Mungu ananisikiliza na kunielewa kuliko mama yeyote kwa mtoto mchanga aliyemzaa na kumpenda. Kwa hiyo atanijibu na kunijalia ninayomuomba walau baadaye kama si mara moja. Hata hivyo nijitahidi kutumia kumbukumbu yangu na ubunifu wangu katika sala, vifanye kazi kwa kunisaidia, la sivyo vitafanya kazi kwa kunizuia nisisali. Nimtegemee hasa Roho Mtakatifu, ambaye yumo ndani mwangu akigusa kumbukumbu ili nikumbuke mambo ya kufaa, na akigusa ubunifu ili nijichoree matukio nisiyoyashuhudia n.k.

Sala ya moyo haitumii akili tu, bali inashirikisha sana utashi, yaani uwezo wa kutaka na kupenda. Roho Mtakatifu akiwa upendo wa Mungu hasa anatuelekeza kwenye upendo: ndiyo sababu kilele cha sala ya moyo ni hatua ya mapenzi. Kwa namna ya pekee Mfransisko anazingatia hatua hiyo. Chini ya imani, kazi ya akili, kumbukumbu na ubunifu ielekee kazi ya utashi ambayo iko chini ya upendo.


5.4. KUKABILI MAGUMU YA SALA


Nikiona nashindwa kukusanya mawazo na kumuambia lolote, na kitabu hakinisaidii, maana yake Mungu anataka kitu kingine kutoka kwangu: nisikubali hata mara moja kishawishi cha kujiona eti, napoteza muda tu, afadhali nifanye kazi nyingine. Siyo kweli hata kidogo. Kukaa na Mungu si kupoteza muda hata kama tunaonekana tumenyamaza wote wawili. Nikiri mbele yake unyonge wangu, nimnyenyekee kwa maneno au kwa kumnyoshea mikono yangu mitupu kama maskini anayeomba msaada nikiamini Mungu hawezi kunikatalia. Naweza pia kukariri maneno machache, k.mf. Bwana unihurumie. Muhimu hasa ni kudumu kwa imani na tumaini hata katika hali ya ukavu.


5.5. KUANDIKA


Kabla sijafunga sala ni vema niandike chochote: muhtasari wake au neno nililolitafakari au sala iliyochipuka moyoni mwangu au azimio nililolifikia au wazo fulani ambalo linaweza kunisaidia hapo baadaye.6. MATATIZO YA SALA YA MOYO

Kama vile kazi yoyote ile, sala ya moyo pia ina matatizo yake. Hasa naweza kupatwa na matatu: kutawanya mawazo, umimi wangu na matakaso ya Kimungu.


6.1. KUTAWANYA MAWAZO


    Hakuna anayeweza kukwepa kabisa tatizo hilo. Kwa wote ni vigumu kukusanya mawazo yamuelekee mfululizo Mungu asiyeonekana wala kusikilikana. Kinyume chake ni rahisi kuacha mawazo yaende huko na huko kama vipepeo. Nahitaji mazoezi mengi, sio wakati wa sala tu, bali saa yoyote; hata hivyo tawanyiko la mawazo litaendelea kunisumbua kwa kiasi fulani. Hilo si dhambi, mradi nisikubali kumsahau Mungu wangu. Pengine ni vizuri nitumie mawazo yanayojitokeza yenyewe na kuyaongelea na Mungu. 
    Nikiona sala inataka kushindikana naweza pia kutumia mbinu mbalimbali. Mojawapo ni kufuata saa kwa kujipangia dakika kadhaa kwa kila hatua ya sala ya moyo: k.mf. dakika moja kwa kuabudu Utatu Mtakatifu, nyingine kwa kujiombea imani, nyingine kwa kumtolea Mungu matendo ya siku nzima, nyingine kwa kumuambia jinsi ninavyompenda n.k. Mbinu nyingine ni kufuata pumzi katika kujiombea neema mbalimbali: k.mf. kuandika maombi kumi ya maadili na kuyatumia mojamoja wakati wa kuingiza hewa mapafuni. 


6.2. UMIMI WANGU


    Kila mmojawetu ana kiasi fulani cha umimi ambao unamfanya ajijali mno. Ndicho kizuio kikubwa kwa sala halisi na maisha maadilifu, kwa kuwa kinasababisha nijifanye lengo la yote badala ya Mungu. Ni lazima nijikane siku kwa siku ili yeye atawale kweli moyo wangu. Sio katika sala tu, bali katika matendo yangu yote nimweke Mungu mbele kuliko mimi na yeyote yule. Litukuzwe jina lake kuliko jina langu, ufike utawala wake kuliko utawala wangu, yatimizwe matakwa yake kuliko matakwa yangu. Nikifaulu kufanya hivyo, sala itakuwa rahisi sana. 
    Kadiri nitakavyoendelea katika njia ya utakatifu nitatambua kuwa ubinafsi huo ni mkubwa mno, nisiweze kuufuta kwa nguvu zangu wala kwa neema za kawaida. Ndiyo sababu natakiwa kutegemea kazi ya Mungu ndani mwangu: yeye anakuja kunitakasa ingawa kwa kunitia uchungu. Daktari wangu huyo ananifanyia operesheni: ndio chanzo cha tatizo la tatu. 


6.3. MATAKASO YA KIMUNGU


    Hayo nayahitaji sana, lakini nisipoelewa chanzo chake na lengo lake yatanikatisha tamaa. Basi, nijue kwamba pengine Mungu mwenyewe anapangua mipango yangu ya sala. Katika matakaso hayo nahitaji uongozi wa kiroho, niambiwe mara nyingi kuwa natakiwa kuendelea kusali hata nikiona eti, ni kazi bure. Nivumilie uchungu wa kibinadamu unaotokana na kazi hiyo ya Mungu. Niamini kuwa faida yake ni kubwa na kuwa baada ya giza kutapambazuka, na baada ya kiangazi mvua itanyesha tena. Nidumu kwa utulivu mbele ya Mungu nikimtolea muda wangu, unyonge wangu na utashi wangu. “Moyo wangu u tayari, ee Mungu, moyo wangu u tayari”. 7. VISHAWISHI VYA KUACHA SALA YA MOYO

Tangu zamani shetani anawashawishi watu wasifanye sala ya moyo, akiwatia hoja zilezile kama kwamba zinatoka akilini mwao. Afadhali nizijue pamoja na majibu ya kufaa nisije nikashindwa na ujanja wake pamoja na udhaifu wangu.


7.1. MBONA SINA MUDA?


    Mtu yeyote, hata akitingwa na shughuli, anaweza na kuhitaji kujipatia nafasi muhimu za kuongea na Mungu, ambaye daima ni wa kwanza katika mafungamano ya maisha. Ni afadhali aache shughuli mbalimbali kuliko sala hiyo. Hapo tunaweza kupima imani yetu: kama tunamzingatia zaidi Mungu au maisha ya hapa duniani. Shida nyingine ni kushindwa kupanga ratiba ya siku. Shughuli zenyewe hazina mwisho, lakini nisiongozwe nazo, bali maisha yangu yote yafuate mapenzi ya Mungu. Hivyo katika mambo yote nitakuwa na mpangilio mzuri, nikifanya kila kitu kwa wakati wake. Tena shughuli zenyewe zinafanyika vizuri zaidi na kwa urahisi zaidi nisipoacha sala ya moyo, kwa sababu inasafisha na kunyosha nia yangu isiwe na mchanganyiko wowote, kama ilivyo kawaida. Kwa mfano, napenda kuokoa watu, lakini pia najisifu nikipata mafanikio; kumbe nitawaokoa kweli ikiwa tu nitaongozwa na upendo. Nisipojipatia muda wa kufanyia sala ya moyo, mwisho nitakuwa kama mtu anayetaka kufanya kazi bila ya kula. 


7.2. MBONA SIPENDEZWI?


    Katika sala ya moyo pengine naonja utamu wa kuwa na Mungu, lakini si lazima wala si muhimu. Lengo si kupendezwa bali kumpendeza. Naye anapendezwa hasa akiniona namuomba kama maskini, ninaposhindwa kusali vizuri na kukusanya mawazo hata nikataka kukata tamaa. Hivyo nikidumu kusali atanijalia neema ingawa kwa siri au baada ya muda. Niwe na imani kuwa Mungu anaona na kujali sio tu mawazo yanayotawanyika, bali hasa hamu na nia yangu ya kukaa naye. Nikiona imani yangu haimpati Mungu, nizidi kumuomba aniongezee imani, badala ya kuacha sala. 


7.3. MBONA SINA MOYO HUO?


Kila mmoja anatakiwa kufanya juhudi alivyotuonya Yesu, katika sala na kazi yoyote, katika kujikana na kubeba msalaba nyuma yake. Kama sina moyo huo, dawa ni kuzidi kumuomba Mungu aimarishe utashi wangu, si kuacha sala.


7.4. MBONA SIJUI?


Ingawa zipo njia mbalimbali za kujifunza sala ya moyo, watu wengi wanyofu wanafundishwa na Roho Mtakatifu mwenyewe. Kila mmojawetu anaweza akajisikia kumfikiria Mungu na matendo yake kwa upendo. Hata hivyo ni vizuri nijifunze njia hizo kutokana na mang’amuzi ya wengine walionitangulia, kwa sababu vilema vinanitawala na pengine nimeanza vibaya.8. MITINDO YA SALA YA MOYO

Njia za kufanya sala ya moyo ni tofauti kwa sababu watu ni tofauti, na kila mmojawetu ana namna yake ya kutenda, kusema, kuwaza na kusali pia. Watakatifu walifundisha kusali walivyozoea na kupenda wenyewe.

Pamoja na hayo, kueleza sala ya moyo ni vigumu kama kueleza kazi ya kupumua: inaonekana kuwa na hatua mbalimbali za kufuata, kumbe ni kitu cha kawaida kwa mtu aliyezoea, asihitaji kuhangaika afikirie hatua hizo.

Mitindo ya sala ya moyo ilifundishwa hasa kuanzia karne ya XVI. Kati yake tunayo hii ifuatayo:


8.1. MTINDO WA KIFRANSISKO (kadiri ya mt. Petro wa Alcantara)


a. kujiandaa

b. kusoma

c. kutafakari

d. kushukuru

e. kumtolea Mungu kitu

f. kuomba.


8.2. MTINDO WA KARMELI


a. Mwanzo

kujiandaa: kumfikiria Mungu kwa upendo, unyenyekevu na tumaini

kujikumbusha lengo: kuwa rafiki wa Mungu

kusoma kidogo

b. Sala yenyewe

kuamini kwamba Mungu yupo

kutafakari somo

kuongea na Mungu kwa upendo au kunyamaza tu mbele yake

c. Mwisho

shukrani kwa neema zote

kumtolea Mungu nguvu zetu katika kumtumikia

azimio na ombi la nguvu za kulitekeleza


8.3. MTINDO WA MT. ALFONSI MARIA


a. Mwanzo

kumuamini Mungu na kumuabudu

kumnyenyekea na kutubu

kuomba mwanga wake

Salamu Maria

b. Sala yenyewe

mawazo mafupi ya imani kwa kutumia pengine kitabu

mapenzi, yaani unyenyekevu, tumaini, upendo, sikitiko n.k.

maombi: ya mwanga, ya kudumu mpaka mwisho na hasa ya kujaa upendo

c. Mwisho

kumshukuru Mungu

kuweka azimio

kuomba neema ya kulitekeleza9. MAMBO YA KUKWEPA KATIKA SALA YA MOYO

Inafaa tusisitize mambo kadhaa yanavyoweza yakazuia sala ya moyo.


9.1. KUJIKAZA MNO


Sala inadai bidii kwa sababu ni kazi ya kumtafuta Mungu. Lakini nisijikaze mno kiasi cha kujichosha kwa muda mrefu. Utulivu wa roho unasaidia zaidi. “Mara nyingi shetani anatushawishi upande huu; asipoweza kufanya tutende mabaya, anatuvuta kutaka tutende mambo makuu kupita uwezo wetu, na kututwisha zaidi na zaidi mpaka tulemewe chini ya mzigo mzito mno” (mt. Vinsenti wa Paulo).


9.2. KUKOSA KIMYA


Nikisema mfululizo sitamuachia Mungu nafasi. Basi niwe tayari kunyamaza akilini na kusikiliza atakayoniambia yeye. “Tunapotaka kumuambia Mungu maneno mengi bila ya kumsikiliza, tunapoteza faida kubwa mno na kuwa viziwi” (mt. Teresa wa Yesu). Maneno ya Mungu yanahitaji nafasi kubwa yaweze kujitokeza.


9.3. KUSINZIA


Nikiri kuwa inaweza ikanitokea kusinzia wakati wa sala. Kama ni hivyo nimnyenyekee Mungu nikikumbuka lawama ya Yesu kwa Petro usiku wa Alhamisi Kuu. Lakini nikiona inanitokea mara nyingi ni lazima nijitahidi zaidi kwa kubadili mtindo wa sala au namna ya kukaa au muda wake. Pengine nahitaji kutibiwa tu.


9.4. KUKATA TAMAA


Nijihadhari sana na kishawishi hicho ambacho Shetani anataka niache sala au niifupishe. Kumbe nikistahimili Mungu ameniandalia neema na anaweza kunimulika kwa mwanga wake. Nikiwa na nia ya kumpenda na kumpendeza kuliko nafsi yangu, itakuwa rahisi kudumu katika sala.


9.5. KIBURI


Mungu anachukia kabisa kilema hicho cha Kishetani. Kujisifia neema zake ni sawa na kukufuru. Kujipongeza ni sawa na kusema uongo. Nipokee neema za Mungu kwa unyenyekevu na kwa mikono miwili. Nikizitumia kwa faida yangu, nisishangae akininyang’anya.


9.6. KUTENGANISHA SALA NA MAISHA


Sala ya moyo inatakiwa kuwa kilele cha bidii zangu zote za kumtafuta Mungu. Vilevile nikitoka kwenye sala nisimuache bali niende naye kwenye shughuli. Hivyo sala ya moyo itapenya maisha yote kwa kuniangazia namna ya kumtumikia Mungu.10. VIPIMO VYA SALA YA MOYO

Naweza nikafikiri kuwa sala ya moyo iliyofanikiwa ni ile yenye mawazo mazuri, kumbe sivyo. Naweza nikaona nimeshindwa kwa sababu ilinibidi nijitahidi mno kukusanya mawazo, kumbe baadaye, wakati wa shughuli, huwa namkumbuka Mungu na kuelewa kwa urahisi ninavyoweza kumtumikia. Hapo nitambue kwamba nimesali vizuri.

Vipimo vitatu vya sala ya moyo ni hivi vifuatavyo:

1. Urahisi wa kumkumbuka Mungu saa zote.

2. Utekelezaji wa wajibu kwa upendo mkubwa.

3. Utayari wa kutumia nafasi za kujikatalia na kumsaidia jirani.

Nikipima sala yangu na kuona sijaendelea vya kutosha, nisikate tamaa, bali nijitahidi zaidi kwa kuwa ndiyo njia ya kujipatia neema nyingi zaidi. Mungu hamuachi mtu anayefanya bidii katika kusali na kutenda mema. Malipo yake yanapita tumaini lolote.