Waklara

Kutoka Wikibooks
Jump to navigation Jump to search

WAKLARA

1. MCHE MDOGO ULIVYOSTAWI (1212-1517)

1.1. MWANZO NA UENEZI (1212-1300)


Mt. Klara, aliyejiita “mche mdogo wa Mt. Fransisko”, ndiye jiwe la msingi la Utawa II ulioleta karama ileile ya Ndugu Wadogo kwa wanawake na kwa kujifungia faraghani. Ndizo nguzo mbili za utawa huo.

Binti huyo wa ukoo bora alizaliwa Asizi (1193). Kisha kuvutiwa na mifano ya Mt. Fransisko, na kusikiliza mahubiri na mashauri yake, akaamua kujiweka wakfu kwa Kristo katika ufukara mkuu. Basi, akatoroka nyumbani usiku (1212) akamuendea Mt. Fransisko huko Porsyunkula ambapo alinyolewa naye na kuvikwa kanzu, kamba na shela nyeusi. Kesho yake asubuhi akapelekwa kwa masista Wabenedikto, na baada ya wiki mbili kwenye monasteri yao nyingine, alipofikiwa na mdogo wake (Mt. Anyesi) ambaye pia alipaswa kukabili upinzani mkali wa ukoo wao. Mt. Fransisko alipomaliza kuandaa jengo la Mt. Damiano, wakahamia huko kushika maisha ya ndani, wakaongezeka haraka. Miaka 40 baadaye Mt. Klara akaja kuandika kwamba mwanzo ulikuwa mgumu na walidharauliwa sana. Mwaka huohuo (au ule uliofuata) mwanzilishi, alipoona walivyovumilia yote, aliwaandikia kwa ufupi “mtindo wa maisha”. Wakati huo aliwaomba wamsaidie kutambua kama Mungu anataka yeye na Ndugu Wadogo waishi upwekeni tu au wafanye utume pia. Jibu likawa kwamba wakahubiri; lakini Mt. Klara na wenzake watawafuata kiroho tu kwa sala na sadaka, wakichangia urekebisho wa Kanisa bila ya kutoka nje ya kiota chao.

Baada ya Mtaguso IV wa Laterano (1215) kukataza kanuni mpya iliwabidi wapokee mojawapo ya zamani ili wakubaliwe na Kanisa kama watawa. Basi wakaichagua ile ya Mt. Benedikto, wakiifuata katika mambo kadhaa kadiri yalivyopatana na mtindo wao mpya, bila ya nia ya kuwa Wabenedikto. Hapo ilimpasa Mt. Klara kuitwa abesi, jina alilolikubali tu kwa kumtii mwanzilishi, ingawa akaendelea kujiita “mtumishi wa Kristo na wa akina dada fukara”. Hasa Mt. Klara hakutosheka na uhalali wa monasteri yake mbele ya Kanisa, bali kwa njia ya Mt.Fransisko aliomba akapewa na Inosenti III “fadhili ya ufukara” (1216), yaani ruhusa ya kuishi bila ya mali hata kijumuia, kama jambo la msingi katika wito wake wa “kuishi kadiri ya ukamilifu wa Injili takatifu”, kwa kuungana na Kristo fukara kama bibiarusi fukara.

Kardinali Ugolino, akiona monasteri za namna hiyo zinavyoongezeka huko na huko, alizitungia katiba (1219) iliyopitishwa na Honori III (1216-1227) ambayo ikawa msingi wa kanuni zote zilizoandikwa baadaye kwa Utawa II. Lengo lake lilikuwa kukinga monasteri hizo dhidi ya upinzani na kuzipa mtindo wa kimonaki zaidi bila ya kuondoa usahili wake maalumu, ziwe muundo mpya wa aina moja chini ya Kanisa la Roma moja kwa moja. Katika juhudi zake za kurekebisha umonaki alielekeza hata monasteri kadhaa za zamani zifuate mtindo wa Mt. Damiano. Desturi kali alizoziagiza humo hazikumtisha Mt. Klara, ambaye alijishinda tayari na kujitesa kwa ushujaa mkubwa (katika kula, kuvaa, kulala n.k.) mpaka akakatazwa asizidishe. Wala hakuogopa ukali wa ugo ulioagiwa na katiba hiyo, ili kutunza mazingira ya sala. Wasiwasi wake ulihusu ufukara mkuu akiona hautajwi na katiba hiyo. Mwanzoni Ugolino alitaka msimamo huo udumu katika monasteri kadhaa, ila alipochaguliwa kuwa Papa akaanza kuzipatia mali nyinginyingi, labda kisha kung’amua matatizo yaliyojitokeza. Lakini Mt. Klara hakukubali kabisa akamuomba amtibitishie “fadhili ya ufukara” akakubaliwa (1228), lakini si kwa monasteri zote.

Suala lingine lililojitokeza mapema, halafu likaendelea kusababisha migogoro, ni nani awajibike kuwasaidia Waklara upande wa roho na upande wa riziki. Mt. Fransisko alipokuwa Mashariki, nd. Filipo Longo aliteuliwa msimamizi wao, lakini mwanzilishi aliporudi uteuzi huo ukafutwa, masista wakasimamiwa tena na wasio Wafransisko, mpaka Gregori IX alipowalazimisha Ndugu Wadogo kuwajibika (1221).

Mt. Klara alipoona wito wake wa Kiinjili upo hatarini upande wa sheria, kwa kuwa kanuni na katiba hazikuwa za Kifransisko, akaanza kuomba aweze kuahidi kushika kanuni ya Ndugu Wadogo badala ya ile ya Mt. Benedikto. Mwaka 1234 akaja kumuunga mkono Mt. Agnesi wa Praha, binti mfalme ambaye alikataa kuolewa na mfalme mkuu Federiko II wa Ujerumani akaanzisha monasteri yake iliyokubaliwa “fadhili ya ufukara”. Alitunga kanuni mpya kwa kuchanganya “mtindo wa maisha” alioandika Mt. Fransisko na katiba ya Ugolino, akamuomba Gregori IX, halafu Inosenti IV waithibitishe, lakini akakataliwa. Kumbe Inosenti IV akathibitisha katiba ya Ugolino (1245) na kusisitiza ifuatwe kanuni ya Mt. Benedikto kwa sababu ina sifa nyingi. Wakati huohuo alijaribu kusuluhisha mgogoro wa uhusiano kati ya Ndugu Wadogo na Waklara. Mt. Klara alikuwa akiendelea kudai kwa nguvu msaada wa kiroho wa ndugu hao kulingana na ahadi ya mwanzilishi. Kumbe Mtumishi mkuu Kreshensi wa Iesi aliomba shirika liondolewe mzigo liliobebeshwa na Gregori IX, yaani himizo la kuanzisha konventi ndogo karibu na kila monasteri ya Waklara. Basi, Inosenti IV aliamua Waklara wawe chini ya uongozi na mamlaka ya Ndugu Wadogo, akapendekeza masista waunganishwe na Utawa I. Lakini shirika likazidi kuona litalemewa na wingi wa monasteri.

Mwaka 1247 Inosenti IV akatunga katiba mpya badala ya ile ya Ugolino iliyokwishaenea katika monasteri zote za Kifransisko, ikitumika pengine pamoja na desturi maalumu za mahali. Katiba hiyo ilifanya kanuni ya Ndugu Wadogo kuwa msingi wa sheria za Waklara bila ya kuwadai waishike katika yote, ila katika utiifu, utovu wa mali na useja mtakatifu. Katiba hiyo ilimuondolea Kardinali mlinzi mamlaka juu ya Waklara, ambao wakawekwa moja kwa moja chini ya viongozi wa Utawa I. Kwa katiba hiyo Waklara wakaja kutambulikana Wafransisko kisheria, lakini ndani mlikuwa na pigo kubwa kwa Mt. Klara, yaani iliandikwa wazi kuwa monasteri zao zinaruhusiwa kuwa na mali za kujitegemea. Ndiyo sababu monasteri chache tu zikaipokea katiba hiyo. Vilevile Ndugu Wadogo wakazidi kulalamika hadi Kardinali mlinzi akajitwalia polepole mamlaka yao na hatimaye (1250) aliwaandikia wasithubutu kujiingiza katika uongozi wa Waklara. Hivyo kwa muda mfupi katiba hiyo ikashindikana pande zote.

Mt. Klara, mgonjwa toka siku nyingi, alipoona kifo kinamkaribia, aliandika wasia wake ambamo alimuiga Mt. Fransisko katika kukumbusha asili ya wito wake na wa jamaa yake, na kutamka kwa msisitizo mkubwa nia imara ya kufuata ufukara mkuu “aliouahidi kwa Mungu na kwa Mt. Fransisko” pamoja na kuhimiza sana umoja wa dada zake. Lakini pia, upande wa sheria, aliona haja ya kutunga upya “mtindo wa maisha” kwa kulinganisha kanuni ya Ndugu Wadogo na masharti ya maisha ya ndani tu. Humo aliingiza pia maandishi mawili mafupi ya Mt. Fransisko kwao, kuhusu ufukara mkuu na kuhusu ahadi ya kwamba yeye na Ndugu Wadogo watawahudumia Waklara sawa na wenzao wa kiume. Upande wake Mt. Klara aliahidi kuwatii waandamizi wa mwanzilishi. Kiini cha huo “mtindo wa maisha” kinasisitiza kwa nguvu nia ya kuishi bila ya mali yoyote, isipokuwa monasteri na bustani. Jambo lingine linalokazwa ni udugu: humo neno “dada” linapatikana mara 66! Udugu huo unatimizwa siku kwa siku chini ya “abesi na mama” kwa umoja wa mioyo pasipo ubaguzi wowote (tofauti pekee ni kati ya wanaojua na wasiojua kusoma kuhusu Sala ya Kanisa). Hata dada “wa nje” (yaani “wanaohudumia nje ya monasteri” bila ya kubanwa na ugo) washiriki maisha ya jumuia sawa na wenzao. Hao ni kundi maalumu la mtindo wa Kiklara, linalohitajika kadiri wenzao wanavyojifungia ndani: ni “akina Marta” kwa “akina Maria” kadiri Mt. Fransisko alivyowapangia Ndugu Wadogo wanaoishi upwekeni. Udugu huo unajitokeza hata katika mikutano, ambayo inatakiwa kufanyika kila wiki kwa mchango wa wote, kupanga shughuli za maana na kuteua watakaoshika nyadhifa mbalimbali. Abesi mwenyewe, ingawa anachaguliwa kwa maisha yake yote, kadiri ya mapokeo ya kimonaki, anaweza kubadilishwa dada zake wakiona hawezi kutimiza vizuri kazi zake. Uhusiano na Utawa I unasisitizwa tena kwa kudai msimamizi wa monasteri awe daima Ndugu Mdogo, pamoja na kuomba Utawa huo uipatie monasteri mapadri 2 na mabradha 2 kwa huduma za kiroho na za kimwili.

Huo “mtindo wa maisha” ukakubaliwa na Kardinali mlinzi (1252) halafu na Inosenti IV (1253). Mt. Klara akapewa hati yake kitandani akaibusu; siku mbili baadaye akafa akiishika mikononi, wakihudhuria nd. Leo, nd. Angelo na nd. Ginepro wenzi wa Mt. Fransisko; pia alijaliwa faraja za Bikira Maria na wanawake watakatifu kadhaa. Mazishi yalihudhuriwa na Papa, Makardinali, Maaskofu na wengineo. Inosenti IV alitaka ziimbwe sala za watakatifu mabikira badala ya zile za wafu, ila akakubali shauri la Kardinali mlinzi la kufuata taratibu zilizopangwa kabla mtu hajatangazwa mtakatifu. Miaka miwili baadaye, Kardinali huyo akiwa amepewa Upapa kwa jina la Aleksanda IV (1245-1261), akamtangaza rasmi kuwa mtakatifu (1255). Mwaka 1260 masalia yake yakahamishiwa mjini Asizi katika kanisa lililojengwa kwa heshima yake.

Pamoja na kanuni na wasia, Mt. Klara ametuachia walau barua nne (kwa Mt. Agnes wa Praha). Maandishi hayo ndiyo chemchemi ya kwanza ambamo tuchote utajiri wa roho yake na wa utu wake. Hasa ya mwisho inatuonyesha alivyogeuka ndani ya Yesu kwa kuzidi kumkazia macho kama kioo chake na kujifunza toka kwake hasa ufukara, unyenyekevu na upendo wa ajabu, vilivyong’aa katika hatua mbalimbali za maisha yake kuanzia Bethlehemu hadi Kalivari. Mt. Klara alimfikia Mungu kwa kumfuata Yesu kama bibiarusi mwaminifu katika hatua hizo za maisha yake halisi, kama alivyoelekezwa na Mt. Fransisko, kadiri ya karama yake mpya katika kumtazama Yesu na kuelewa Injili.

Katika karne ya XIII monasteri chache ziliipokea kanuni ya Mt. Klara iliyothibitishwa kwa ajili ya nyumba asili tu. Kumbe monasteri kadhaa zikaja kupokea kanuni maalumu ambayo M.H. Izabela (+1270), dada wa Mt. Ludoviko IX mfalme wa Ufaransa, aliiandika akakubaliwa na Aleksanda IV kwa monasteri yake ya Longchamp (1259). Kanuni hiyo iliweka Waklara chini ya Ndugu Wadogo na kukubali mali na mapato ya mara kwa mara.

Mwaka 1263 mkutano mkuu wa Ndugu Wadogo ulizidi kukataa wajibu wa kuwahudumia Waklara. Akiwa Mtumishi mkuu, Mt. Bonaventura alijaribu kusuluhisha kwa kusema huduma za kiroho kwa dada hao zinatokana na upendo, lakini si wajibu ambao waudai kwa haki; pia zitegemee uamuzi wa Kardinali mlinzi. Kumbe mwaka huohuo Urbani IV (1261-1264) alipitisha kanuni mpya ili kustawisha nidhamu na. umoja ikidai monasteri hizo zote ziitwe Utawa wa Mtakatifu Klara (O.S.C.), kama ilivyoelekea kufanyika baada ya kutangazwa mtakatifu. Kanuni mpya ilifuata kidogo ile ya Klara, na zaidi katiba ya Inosenti IV, ikibana sana masista katika vipengele vingi. Zaidi ya hayo ilipanga mali (mashamba na kodi zake) kuwa tegemeo la kawaida la uchumi wa monasteri. Hatimaye iliwaondolea Watumishi wajibu wa kuwahudumia Waklara. Kanuni hiyo ikakataliwa na monasteri bora na baadhi ya Ndugu Wadogo. Hivyo ukatokea mgawanyiko unaodumu hadi leo kati ya Waklara wanaofuata kanuni ya Mt. Klara (inayoitwa ya I) na wale wanaofuata kanuni ya Urbani IV (Waurbani au wa kanuni ya II), na kufanana na Wakonventuali (ambao pia wamekubali kuwa na mali kishirika). Kanuni nyingine zikaachwa kabla ya karne kwisha. Kwanza ilienezwa sana ile ya Urbani, lakini ile ya mt Klara ikabaki huko na huko ikiendelea kuathiri sana historia yote ya Waklara kwa kukumbusha tunu asili na kuchochea marekebisho mengi kuliko yale ya Ndugu Wadogo, kutokana na urahisi wa kubadili hali ya monasteri moja kuliko ya shirika kubwa iliyotawanyika sehemu mbalimbali.

Tofauti hizo hazikuzuia uenezi wa monasteri usiende kasi ajabu, kulingana na uenezi wa Utawa I Ulaya na hata ng’ambo ya Bahari ya Kati. Kila monasteri ilijitegemea kikamilifu; kilichowaunganisha ni hakika ya kutokana na moto ule uliowashwa na Mt. Klara, uhusiano wa kiroho na Ndugu Wadogo na mamlaka ya Kardinali mlinzi. Kwa kawaida monasteri zilikuwa na masista wengi sana. Miito mingi ilitokea kati ya koo maarufu na za kifalme pia, hasa Urbani IV alipodai kila mtakaji alete “mahari” monasterini, sheria ambayo ilienea kote. Karne ya kwanza ilizaa watakatifu 4 (Klara na Agnes wa Asizi, Agnes wa Praha na Kinga wa Hungaria) na wenye heri 6 katika nchi mbalimbali, hasa kutoka koo za kifalme. Halikukosekana taji la ushahidi wa imani na wa ubikira (Waklara wote wa Tripoli mwaka 1289, na wote 70 wa Tolemais mwaka 1291).

Takwimu ni kama ifuatavyo:Mwaka 1253 
Mwaka 1300 

Waklara

Zaidi ya 15,000 

Monasteri

111 
413 

 Italia + visiwa 
68 
196 

 Hispania + Ureno 
21 
57 

 Ufaransa 
14 
68 

 Ujerumani + Ulaya Mashariki 
8 
46 

 Mashariki + Korasia 
 
23 

 Uingereza + Irelandii 
 
23 


1.2. ULEGEVU (1300-1400)


Karne ya XIV ilileta ulegevu katika Utawa II, kama tulivyoona kwa ule wa kwanza, hasa kutokana na wingi wa masista na wa mali. Walipokewa kwa urahisi wanawake wasiofaa lakini wenye kuleta mahari kubwa, ambao waliingiza monasteri watumishi wao binafsi, hata kuleta anasa, pengine kwa idhini ya Papa. Uovu ulizidi wakati wa farakano la Magharibi na fujo iliyofuata. Hata hivyo si monasteri zote zilipatwa kwa pamoja, kutokana na kila moja kujitegemea. Hazikukosekana pia juhudi za kurudisha nidhamu zilizofanywa na wasimamizi wa Utawa I – ambao Bonifas VIII (1295-1303) aliurudishia wajibu wa kuwahudumia Waklara (1296) – na Makardinali walinzi na Mapapa wenyewe. Kati yao ni muhimu hasa Benedikto XII (1334-1342), aliyekuwa mmonaki wa Citeaux, ambaye aliwapa Ndugu Wadogo katiba (1336) ambayo sura yake mojawapo inahusu Waklara tu. Katiba yake ilibadili sura ya monasteri. Kwanza ilipanga idadi ya juu ya masista katika kila monasteri; pili ilisisitiza ugo wa Kipapa, taratibu za pamoja kwa wote, usimamizi mzuri wa mali, katazo la pesa za binafsi na la dhuluma dhidi ya monasteri; tatu alilazimisha hata dada waliohudumia nje ya ugo wabaki ndani na hivyo wakaja kuwa tabaka la chini masista, wakiwatumikia wenzao bila ya kuwa na sauti mikutanoni (ilikuwa hivyo kwa Wabenedikto, lakini ni kinyume cha udugu alioutaka Mt. Klara); nne kwa huduma hizo za nje waliruhusiwa wanawake wasekulari wa kufaa; tano vilikatazwa vyumba vya binafsi.

Jambo lingine lililokuja kubadilishwa ni muda wa uongozi wa abesi, kwa kuzingatia kwamba urefu wake unaweza ukafaa wakati wa juhudi, lakini unaweza ukasababisha uharibifu wa kudumu ulegevu ukiingia. Mtindo wa maisha wa Mt. Klara hausemi abesi adumu muda gani, ila unafuata kanuni ya Mt. Fransisko ukisema asipofaa tena aondolewe, halafu achaguliwe mwingine. Lakini utekelezaji wake haukuwa rahisi. Hivyo Inosenti VII (1404-1406) aliagiza (1405) abesi achaguliwe kila baada ya miaka 10; baadaye muda ukapunguzwa tena hadi miaka 3. Lakini sheria hizo hazikufuatwa popote, hivyo baadhi ya monasteri zikaendelea kumchagua abesi hadi atakapokufa.

Pamoja na juhudi hizo na nyingine za kurekebisha hali, historia ya watawa inaonyesha kwamba nidhamu ya kuzalimishwa inaweza ikasidia kiasi, lakini haiwezi kuleta hali mpya, kwa kuwa uhai unatoka ndani ya watawa wenyewe kwa kazi ya Roho Mtakatifu. Si suala la miundo, bali la roho. Hata katika ulegevu wa karne ya XIV mtindo wa maisha wa Mt. Klara ulivutia: kwa mfano malkia Sancha wa Napoli (+1345), alipojifanya Mklara hakukubali kuingia monasteri ya fahari ya Mt. Klara mjini, bali alianzisha nyingine ndogo fukara kwa kuita wamonaki toka Asizi na kushika kanuni ya I. Huko na huko Ufaransa ilitokea vilevile. Katika karne hiyo walipatikana wenye heri 3.

Takwimu ni kama ifuatavyo:Mwaka 1300 
Mwaka 1385 

Waklara

Zaidi ya 15,000 
Zaidi ya 15,000 

Monasteri

413 
404 

 Italia + visiwa 
196 
245 

 Hispania + Ureno 
57 
51 

 Ufaransa 
68 
39 

 Ujerumani + Ulaya Mashariki 
46 
50 

 Mashariki + Korasia 
23 
11 

 Uingereza + Irelandii 
23 
8 


1.3. MAREKEBISHO KUANZA (1400-1517)


Karne ya XV hadi ya XVIII ziliona monasteri za Waklara kuhuishwa tena, kufuatana na marekebisho ya Ndugu Wadogo (kama ilivyotokea kwa wanawake wa mashirika mengine), halafu na Mtaguso wa Trento na maagizo ya Mapapa, lakini pia kutokana na karama yenyewe ya Mt. Klara iliyojitokeza wazi katika kanuni yake. Toka mwanzo utawa wake haukuwa tu muundo mpya wa kimonaki, bali mfumo mpya wa maisha ya Kiinjili, ambao unadai kufuatwa, la sivyo monasteri hazitatulia, kama vile Ndugu Wadogo.

Mwanzoni mwa karne ya XV ulitokea urekebisho mkubwa kwa njia ya Mt. Koleta Boylet (+1447) wa Corbie (Ufaransa). Baada ya kujifungia ndani amevaa mavazi ya Wafransisko Wasekulari, alitokewa mara kadhaa na Mt. Fransisko na kuhimizwa arekebishe utawa wake. Basi, akatoka (1406) akaenda kwa Papa wa Avignon (bila ya kutambua kwamba ni wa bandia) akaweka mikononi mwake nadhiri ya kushika mtindo wa maisha wa Mt. Klara, akafanywa naye abesi na mrekebishaji wa utawa wote wa Mt.Fransisko (I-II-III), kutokana na karama yake wazi ya kurekebisha Kanisa kuanzia monasteri na miundo mingine ya Kifransisko. Kwa neema ya Mungu na kwa msaada wa wakuu wa dunia akaanza kutembelea Ufaransa na Benelux ili kueneza chachu ya Kiinjili, hasa ufukara. Upande wa Waklara alirekebisha au kuanzisha monasteri 22 kufuatana na kanuni ya I aliyoomba nakala yake halisi kwa monasteri mama ya Asizi. Mwenyewe aliiongezea katiba iliyopitishwa na Mtumishi mkuu (1432) halafu ikathibitishwa na Pius II (1458-1464). Humo alikataza mahari za masista, mali yoyote na mapato ya hakika kwa monasteri, kodi na ghala za kutosha muda mrefu, kila kitu cha thamani au kisicho cha lazima, majengo yasiyo duni. Aliagiza wote wafanye kazi ili kupata riziki, bila ya kuagiza watu wa nje kwa kazi wanazoweza kuzifanya wenyewe. Kwa udogo, alikataza baraka kuu kwa abesi na ibada ya kuweka wakfu mabikira. Hata hivyo alisisitiza usafi na masomo na kupunguza masharti ya ugo. Kwa ajili ya upendo wa kidugu alifuta matabaka, aliagiza vipindi vya burudani (maongezi), alisisitiza mikutano ya kila wiki, alionyesha tena kuwa wadhifa wowote ni utumishi tu. Ingawa alikubali vipengele kadhaa vya kanuni ya Urbani IV vilivyopata kuwa vya kawaida, kwa jumla alirudia vizuri karama ya Mt. Klara. Kama yeye alitaka mafungamano imara na Utawa I, monasteri zote zikiwa chini ya Ndugu Wadogo, na wanne kati yao wakiwa tayari kuihudumia kila mojawapo. Kwa sababu hiyo, kama tulivyokwishaona, watawa kadhaa wa kiume waliingia katika juhudi zake za urekebisho (Ndugu Wadogo Wakoleta).

Waoservanti mwanzoni walikataa kuwahudumia Waklara, lakini polepole wakalazimishwa na Kanisa kwa ombi la monasteri zilizorekebishwa. Hapo urekebisho wa kina ukapamba kwa juhudi za wamonaki bora, kama Mt. Katerina wa Bologna (+1463), M.H. Antonia wa Firenze (+1472), Mt. Eustokia Calafato (+1485) na M.H. Batista Varano (+1524) huko Italia, na wengineo Ufaransa na Hispania. Wote walishikilia kanuni ya I sio tu kwa Waurbani, bali pia kwa monasteri nyingi za Utawa III na hata nyingine zisizokuwa za Kifransisko! Si zote zilikubali kwa ridhaa yao urekebisho. Kumbe Waoservanti walijaribu kuueneza kote, hata kwa mabavu, mpaka walifikia hatua ya kutumia nguvu za kijeshi kupitia serikali! Kati ya wote aliyejitahidi zaidi ni Mt.Yohane wa Capestrano, ambaye alitaka pia kuunganisha monasteri zote chini ya Waoservanti, lakini akashindana na msimamo wa mt Koleta aliyetaka kubaki chini ya Mtumishi mkuu na kudumisha uhusiano na Wakonventuali. Mt.Yohane akaandika (1445) ufafanuzi wa kanuni ya Mt. Klara akiorodhesha amri mia na zaidi, jambo lililowashangaza sana Waklara, hata mwaka uliofuata ulitolewa ufafanuzi mwingine juu ya maana ya amri hizo, halafu Eugeni IV (1431-1447) akatamka kwamba chache tu zinawabana masista kiasi cha kutenda dhambi wakizivunja (1447). Mwenyewe aliweka chini ya Waoservanti monasteri zote zilizorekebishwa, hata zikifuata kanuni ya II, akiziacha nyingine chini ya Mtumishi mkuu. Kwa maana sera ya Kanisa haikuwa kulazimisha monasteri kufuata kanuni ya I, ila kuzirekebisha kwa kufuata sawasawa sheria za kila mojawapo; pengine waliokataa urekebisho iliwabidi wahame. Mwishoni mwa karne ya XV Waklara wa urekebisho wakawa wengi kuliko wasiorekebishwa. Sehemu nyingine monasteri za hawa wa mwisho zilikuwa na hali mbaya kweli. Hatimaye baadhi ya zile zilizokataa urekebisho zilibadili kanuni na kufuata ile ya Mt.Benedikto. Jambo lingine lisilopendeza lilikuwa kuona Waoservanti na Wakonventuali wakishindania monasteri za dada zao.

Kati ya marekebisho hayo, Wakoleta wamedumisha hadi leo umoja fulani kati ya baadhi ya monasteri zao. Vilevile Waklara Pekupeku walioanzishwa na Marina wa Villaseca (Hispania) aliyeruhusiwa (1490) kurekebisha monasteri yake ya Utawa III kwa kufuata kikamilifu kanuni ya I, na kupokea Waurbani wasirudie unovisi. Makundi mengine yamepoteza umaalumu wao: kwa mfano Dada Fukara Waklareno ambao Sisto IV aliwaweka (1473) chini ya Mtumishi mkuu kumpitia makamu wake Mklareno.

Inosenti VIII (1484-1492) alimruhusu (1489) mt Beatriche wa Silva Meneses (+1490) aunde monasteri ya Kibenedikto aina ya Citeaux kwa heshima ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi Asili (Imaculata Concepcion). Baada ya mwanzilishi kufariki, Aleksanda VI akawaruhusu hao masista Wakonsesioni wafuate kanuni ya Mt.Klara na kuunda monasteri nyingine, halafu Julius II (1503-1513) akawapatia kanuni mpya (1511) ambayo inafanana nayo, lakini inaruhusu mali ya monasteri na kulegeza mfungo. Hata hivyo wakaachwa chini ya Ndugu Wadogo wakapewa fadhili zote za Waklara (1520). Ndiyo sababu wanaorodheshwa pamoja na Utawa II. Hao wakastawi sana Ulaya na Amerika hadi leo.

Tofauti zaidi ni Utawa wa Bikira Maria (Waanunsyata) ulioanzishwa na malkia Mt. Yoana wa Valois (+1505) kwa heshima ya Maria Mpashwa Habari. Tawi hilo halifuati kanuni ya Kifransisko, lakini toka mwanzo liko chini ya Waoservanti na linashiriki fadhili za Waklara: ndiyo sababu linaorodheshwa pamoja nao.

Katika kipindi hicho ni vigumu sana kutoa takwimu za idadi ya masista. Kati yao, mbali ya watakatifu 5 waliotajwa, walipatikana wenye heri 7.2. MAREKEBISHO KUENDELEA (1517-1762)

Baada ya utengano wa Ndugu Wadogo (1517) monasteri zilizo nyingi ziliwekwa chini ya Waoservanti, hata zile za Wakoleta (nyingine tena zikaongezwa baadaye, k.mf. zile zote za Hispania na Ureno mwaka 1566). Kama kawaida mzigo huo ulilalamikiwa na mkutano mkuu (1532); hivyo ikakatazwa monasteri nyingine zisipokewe chini ya OFM pasipo ruhusa ya mkutano, na hasa wahusika washughulikie mahitaji ya kiroho tu ya Waklara. Baada ya Mtaguso wa Trento kutoa maagizo kuhusu watawa wanawake (1563) yaliyochangia marekebisho ya sheria na hasa juhudi kwa maisha magumu, mkutano mkuu wa OFM ulitunga sheria muhimu kwa utekelezaji wake ukifuta wadhifa wa ndugu msimamizi wa Waklara na kuwaweka moja kwa moja chini ya Watumishi wa kanda (1565). Lakini Waoservanti walipojaribu kusawazisha mno, kwa kudai monasteri zote ziwe na mali (ilivyoruhusiwa na Mtaguso) wakapatwa na matatizo makubwa, hasa kwa sababu Wakoleta hawakukubali kuacha ufukara mkuu, na kuja kulingana na Waurbani wenye kutegemea mali zao.

Urekebisho wa Ndugu Wadogo Wakapuchini ulisababisha mapema tawi jipya la Waklara linalodumu hadi leo. Mwanzilishi ni Maria Lorenza Llonc (+1542) mjane Mhispania aliyeishi Napoli (Italia) na kuhudumia wagonjwa pamoja na jumuia ya wanawake Wafransisko wasekulari aliyoianzisha. Wakapuchini walipohamia hospitali yake (1529), akawakabidhi uongozi wa jumuia hiyo. Kati ya 1533 na 1538 wakaongozwa na Mt. Gaetano wa Thiene aliyewaelekeza kwenye maisha ya sala tu na kuwatafutia idhini ya kuishi kimonaki kwa kufuata kanuni ya Mt. Klara (1535). Baadaye akawakabidhi tena Wakapuchini, kwa kuwa karama yao iliathiri sana monasteri hiyo na roho yake, na ndivyo alivyotaka mwanzilishi. Paulo III (1534-1549) akathibitisha hayo na nia yao ya kushika kikamilifu kanuni (1538). Kwa ajili hiyo mwanzilishi aliikamilisha katiba ya Mt. Koleta kwa kutumia ile ya Wakapuchini. Sifa ya monasteri ikaenea haraka na kusababisha kabla ya 1600 zianzishwe 17 nyingine Italia (Mt. Karolo Boromeo aliunda tatu katika jimbo lake). Ila Wakapuchini wanaume wakakataa katakata kuzisimamia, isipokuwa mbili. Hata hivyo dada zao wakaendelea kuomba msaada huo kwa kuwapitia Maaskofu na wafalme, mpaka Mapapa wakalazimisha hao wanaume kuhudumia walau kiroho monasteri fulanifulani. Hata nje ya Italia wakaenea haraka: Hispania (1588), Ufaransa (1603), Ureno(1625), Mexico(1665) ambayo ikawa nchi walipoongezeka zaidi hadi leo, Peruu (1713), Gwatemala (1725), Chile (1727) n.k.

Hata marekebisho mengine ya Utawa I yalijaribu bure kukataa huduma kwa Waklara, hasa Wariformati waliojitahidi sana ili Mapapa wawaweke wote chini ya Maaskofu. Hatimaye wakalazimika kuwahudumia Waklara. Masista wa Utawa II na III waliokuwa chini ya Warekoleti wakaja kutumia jina hilo pia.

Marekebisho mengine ya Waklara yalifanyika katika karne ya XVII, hasa Italia. Kati yake ule wa Wakaapweke wa Mt. Petro wa Alkantara, ulioanzishwa na Kardinali Mkapuchini na kuthibitishwa na Klementi X (1670-1676), ndio tawi gumu kuliko yote yaliyowahi kuwepo. Masista hao waliishi kila mmoja peke yake kama Wakartusi na kujitahidi kumuiga Mt. Petro wa Alkantara katika yote, lakini hawakuenea sana.

Katika karne ya XVII na XVIII hata Waurbani wakapata marekebisho yao hasa upande wa ufukara, Ufaransa na Italia.

Waklara waliorekebishwa walitoa mifano bora ya kutetea imani na ubikira wakati wa uenezi wa Kiprotestanti na vita vya dini vilivyofuata. Upungufu uliosababishwa na mambo hayo Ulaya Kaskazini ulifidiwa kabisa sio tu katika nchi zilizobaki kuwa za Kikatoliki, bali hata Amerika na Asia. Wakonsesioni walifika Mexico mwaka 1540. Waklara wakafungua monasteri yao ya kwanza ya Amerika huko Hispaniola mwaka 1551. Monasteri nyingine zikaanzishwa karne hiyohiyo Peruu, Ekwado, Kolombia, Chile, Gwatemala na Brazili. Katika karne ya XVII Waklara wakaenea Filipino (1621) na China (1633). Katika karne ya XVIII ongezeko liliendelea ingawa kasi yake ilipungua. Takwimu ni kama ifuatavyo:Mwaka 1587 
Mwaka 1680 

Waklara tu

28,000 
38,000 

Monasteri zao

618 
973 

 Hispania + Ureno 
277 
394 

 Italia + visiwa 
199 
248 

 Ufaransa 
91 
182 

 Ulaya ya Kati 
46 
128 

 Amerika 
5 
21 

Monasteri za Wakonsesioni

76 
90 

Monasteri za Waanunsyata

9 
40 


Kati yao wote anang’aa hasa Mt. Veronika Giuliani (+1727) aliyejaa karama na njozi tangu utotoni, alivyosimulia kwa utiifu na unyofu katika shajara yenye kurasa 22,000. Wako pia wenye heri 4.3. KARNE ZA MWISHO (1762-2005)

Kama ilivyowatokea Ndugu Wadogo, Waklara pia walishambuliwa na siasa mpya za serikali, kuanzia Austria na nchi zote zilizokuwa chini yake (1782-1783), monasteri zote zilipofutwa. Uamuzi huohuo ulichukuliwa Ufaransa (1792); miaka 2 baadaye M.H. Yosefina Leroux akauawa kwa kosa la kuanza tena kuishi kijumuia), halafu Ubelgiji, Italia, Ujerumani na Hispania. Katika nchi hiyo ya mwisho monasteri nyingi zikaendelea hata baada ya sheria nyingine kudai zifutwe; pengine ilitumika mbinu ya kukubali kutoa huduma fulani (k.mf. shule) Lakini katika nchi nyingine monasteri nyingi zikaisha, hasa Ureno ambapo zilikwisha zote kufuatana na sheria ya mwaka 1834.

Tangu miaka ya kwanza ya karne ya XIX monasteri zikaundwa tena Ufaransa na Ubelgiji, pamoja na kuanzishwa mashirika mengi ya Kifransisko. Mojawapo ni tunda la Maria Klara Bouillevaux (+1871) aliyelianzisha Paris (1854), likifuata kanuni ya Utawa Hasa III na katiba maalumu, yenye jambo la pekee la kuabudu ekaristi saa zote. Mwaka 1912 monasteri zake zote zikapokea kanuni ya Urbani IV na kujiita Waklara Fukara wa Kuabudu Mfululizo, halafu Wafransisko wa Sakramenti Kuu. Walienea sana na kudumisha uhusiano na Wakapuchini. Hata katika nchi nyingine monasteri mpya ziliundwa na nyingine zilifunguliwa tena. Baadhi ziligeuka kuwa mashirika ya kitume, bila ya kuacha kanuni ya Kiklara.

Katika karne ya XX uenezi ukaendelea hasa katika nchi za Amerika na za misheni. Baada ya Mkusanyo wa Sheria za Kanisa idara ya Papa kwa Watawa iliagiza itungwe katiba moja kwa Waklara wote, isipokuwa Wakapuchini. Kazi hiyo ilifanywa polepole na OFM kwa kupokea mapendekezo ya maabesi pia, ikapitishwa (1930), lakini si kwa Wakoleta. Kwa Waklara Wakapuchini katiba ilitungwa na wenzao wa kiume na kupitishwa mapema zaidi (1927). Waurbani pia wakaja kukubaliwa katiba maalumu (1973). Juhudi hizo za kuimarisha umoja zilichangiwa sana na Pius XII (1939-1958) alipohimiza mashirikisho ya monasteri pamoja na kulegeza masharti ya ugo (1950) kwa lengo la kuziondoa katika hali ya ukiwa, kuzisaidia upande wa malezi na kuruhusu pengine uhamisho. Kazi hiyo ilianza Ufaransa (1953) na kuendelezwa na Mtaguso II wa Vatikani hivi kwamba mwaka 1975 kulikuwa na mashirikisho 43 (1 chini ya Wakonventuali, 7 ya Wakapuchini na 35 ya OFM). Ni mafanikio makubwa tukizingatia ugumu wa kushinda desturi za siku nyingi na tofauti za kila aina. Uhusiano kati ya monasteri na kati ya hizo na Wafransisko wengine umeongezeka na kuinua ujuzi wa kidini na wa hali na mahitaji ya Kanisa na ya ulimwengu. Mtaguso uliagiza pia matabaka kati ya masista yafutwe; hivyo Waklara wakarudia mpango wa mwanzilishi kuhusu udugu, pamoja na kuzidi kuchimba karama yake kwa jumla. Katika uchangamfu huo mpya monasteri nyingi zikapokea kanuni ya I badala ya ile ya II. Hivyo mnamo mwaka 1975 kati ya monasteri za Waklara, 660 hivi zilikuwa zinafuata kanuni ya I na 150 hivi ile ya II. Hata sinodi ya Maaskofu kuhusu watawa (1994) ikajadili sana masuala ya wamonaki na kuhimiza tena mashirikisho yaimarishwe na ugo urekebishwe hasa kwa faida ya malezi.

Baada ya ongezeko la nusu ya kwanza ya karne ya XX, uhaba wa miito Ulaya umerudisha nyuma ustawi wa monasteri nyingi. Takwimu ya uenezi ni kama ifuatavyo:Mwaka 1907 
Mwaka 1980 
Mwaka 2005 

Waklara tu

11,000 
17,000 
12,593 

Monasteri zao

561 
824 
930 

 Hispania + Ureno 
185 
289 
 

 Italia 
157 
144 
 

 Amerika 
40 
172 
 

 Ulaya ya Kati 
53 
78 
 

 Asia + Afrika + Australia 
 
60 
 

 Ufaransa 
43 
52 
 

Monasteri za Wakonsesioni

88 
153 
157 

Monasteri za Waanunsyata

6 
4 
8 


Kuhusu matawi, mwaka 2005 takwimu zilikuwa hivi:Watawa 
Monasteri 

Waklara wa kawaida

7,662 
569 

Waklara Wakoleta

681 
57 

Waklara Waurbani

1,122 
86 

Waklara Wakapuchini

2,246 
162 

Wakapuchini wa Sakramenti Kuu

295 
22 

Waklara wa Kuabudu Mfululizo

587 
34 

Jumla ya Waklara

12,593 
930 

Wakonsesioni

2,019 
157 

Waanunsyata

96 
8 


Waklara wafiadini wengine 6 wa karne ya XX, hasa Wahispania, wameshatangazwa wenye heri. Mklara maarufu zaidi wa milenia mpya ni sr. Maria Anjelika wa Kupashwa Habari ambaye, karibu na monasteri yake ya kuabudu ekaristi mfululizo, ameanzisha (1981) mtandao wa Kikatoliki mkubwa kuliko yote ya Amerika (EWTN)!