Historia ya Utawa

Kutoka Wikibooks

Maisha ya kitawa yanapatikana katika dini mbalimbali. Hapa tutazungumzia aina zake tofauti zilizojitokeza katika Kanisa kadiri ya wakati na mahali mbalimbali ambapo Roho Mtakatifu aliwakirimia watu wake wajitoe kabisa kwa ufalme wa Mungu nyuma ya Yesu. Hatuwezi kuelewa utawa tukidhani ni kitu kimoja, bali jina hilo linajumlisha maisha ya aina nyingi yanayomshuhudia Kristo katika sifa na kazi zake mbalimbali.

Tunataka kufuata historia ya maisha hayo kama kitabu bora kilichoandikwa na Mungu siku kwa siku kadiri ya mpango wake wa hekima kwa ujenzi wa taifa lake takatifu. Kuna hatua kuu nne ambazo zilizaa mitindo mipya zaidi, hasa upande wa Magharibi, lakini bila ya kufuta ile iliyotangulia:

1. Hadi karne ya XII ulitawala mtindo wa kimonaki ukifuatwa na ule wa kikanoniki (Bazili, Benedikto na Norberti ndio watakatifu maarufu zaidi).

2. Kati ya karne ya XIII hadi ya XV yalitokea mashirika ya waombaomba (Fransisko wa Asizi na Dominiko ndio watakatifu wakuu).

3. Kati ya karne ya XVI hadi ya XIX yalitokea mashirika mengi ya wakleri wafuatakanuni, ya maisha ya kitume na ya watoahuduma (Ignasi wa Loyola ndiye mtakatifu muhimu zaidi).

4. Hatimaye karne ya XX imeona uanzishaji wa mashirika ya kilimwengu na wa jumuia za aina mpya.


MWANZO: UBIKIRA NA JUHUDI NYUMBANI

Kufuatana na mifano ya Bikira Maria na hasa ya Yesu Kristo, tunasoma katika Agano Jipya habari za wanaume na wanawake waliojinyima ndoa kwa ajili ya ufalme wa Mungu, kama vile mabinti wanne wa shemasi Filipo waliokuwa mabikira na manabii (Mdo. 21:9). Hasa mtume Paulo aliwahimiza Wakristo wowote wanaoweza wafanye hivyo kama alivyofanya mwenyewe kufuatana na shauri la Bwana (taz. 1Kor. 7:25-34).

Hata katika maandishi ya mababu wa Kanisa kuanzia karne ya I tunasoma sifa za watu wa toba wanaozungukazunguka ili kuhubiri na za mabikira ambao utakatifu wao unaonyeshwa kama alama ya ubora wa Ukristo juu ya ulimwengu wa anasa unaoliudhi Kanisa. Polepole mabikira hao walianza kuorodheshwa na kukubaliwa na Askofu na kukusanywa katika jumuia (utawa wa mabikira). Ilitokea vilevile kwa wanaume wa toba walioanzisha miundo kamili kuliko juhudi za nyumbani mwao, wakishika ufukara fulani wa hiari, mafungo, kujinyima vyakula mbalimbali, kukesha usiku, kuimba Zaburi na kusali kwa moyo.



UMONAKI NA KUKIMBIA ULIMWENGU

Tofauti na watu waliotangulia ambao waliishi katika mazingira ya kawaida, mwishoni mwa karne ya III huko Misri ulianza mtindo wa kukimbia ulimwengu hata kimakao (umonaki, kutoka neno la Kigiriki monos = mmoja). Mmonaki alitafuta upweke kamili hasa jangwani ili kuishi na Mungu tu, bila ya kushikwa na mitindo na masharti ya maisha ya kawaida ili moyo uweze kutulia kabisa na kumpenda Mungu bila ya kugawanyika. Miundo mipya ya umonaki ilitegemea matatu: mwanzilishi, kanuni, upweke. Mtindo huo wa maisha, ambao ndio mchango mkuu wa Afrika kwa Kanisa lote, ulistawi hasa baada ya dola la Kirumi kuruhusu Ukristo mwaka 313.

Anayeheshimiwa kama baba wa wamonaki ni mt. Anthoni abati (251-356) ambaye akizingatia maneno mbalimbali ya Injili aliwagawia maskini utajiri wake mkubwa amfuate Mwokozi. Maisha yake yote akazidi kujitafutia mahali pa upweke kamili zaidi ili kumtafuta Mungu tu. Mfano wake ulivuta wanaume na wanawake wengi sehemu mbalimbali, naye Anthony aliwaongoza bila ya kuacha upweke wake. Maisha magumu ya makundi hayo yaliamsha Kanisa lifuate Injili kwa juhudi kama wakati wa dhuluma, ambapo ulihitajika ujasiri mbele ya hatari ya kuuawa. Hivyo umonaki ulionekana aina mpya ya kifodini kwa jinsi ulivyomtolea Mungu maisha yote.



MAISHA YA PAMOJA MASHARIKI

Muda mfupi baadaye, na sehemu ileile, yalianzishwa maisha ya pamoja ambamo mali na vilevile mang’amuzi ya Kiroho yashirikishwe, hata mna mwanzo wa kushughulikia watu wa ulimwenguni.

Mt. Pakomi (288-346) aliongokea imani kwa kuzingatia Wakristo walivyowatumikia wafungwa kwa upendo. Mang’amuzi hayo yalimuangazia kuwa Mungu ni upendo na kama kawaida yaliathiri maisha na mafundisho yake yote. Hivyo baada ya kushika umonaki akajisikia wito wa kuishi kwa upendo na wengine akaanzisha maisha ya pamoja upwekeni huko Misri Kusini. Ndiye wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa, na ndani yake jina “ndugu” linashika nafasi ya “mmonaki”. Kanuni hiyo ikaja kupenya maisha ya wamonaki na kanuni Mashariki na Magharibi vilevile. Mbali ya mafungo na sala ndefu, Pakomi alisisitiza kujikana kwa ajili ya wengine, yaani kuwa na utiifu, huruma na misaada ya kila aina: ndiyo njia ya upendo ambayo iliagizwa na Bwana na kufanya maisha ya pamoja yawe bora kuliko upweke kamili. Karibu na monasteri za kiume kuliko na nyingine za kike.

Pia mt. Bazili Mkuu (330-379) alianzisha maisha ya pamoja baada ya kutembelea wamonaki sehemu mbalimbali. Aliita monasteri “jamaa” kwa kuwa lengo lake kuu lilikuwa kushika kikamilifu udugu wa Kiinjili kama katika Kanisa la mwanzoni. Tofauti na monasteri ya Pakomi iliyofikia kuwa na maelfu ya wamonaki, jamaa hiyo haikuwa kubwa sana wala kuwa na ngome, wala kuishi jangwani, bali karibu na mji wa Kaisarea wa Kapadokia. Akiwa askofu huko alisisitiza uhusiano na Kanisa: wamonaki wa kiume na wa kike wawe chachu inayofanya Wakristo wenzao wafuate utakatifu wa wito wao, tena aliwakabidhi shughuli mbalimbali kama kuhubiri na hasa kuhudumia wenye shida. Mtindo wake ulisisitiza ushirikiano kati ya ndugu kuliko uongozi wa abati na miundo mikubwa. Mpaka leo kanuni zake zinaongoza karibu wamonaki wote wa Mashariki, na kwa njia yao makanisa ya Orthodoksi kwa kuwa maaskofu kwanza ni wamonaki nao wanaelekeza wakristo wote kufuata mifano yao.



MAISHA YA PAMOJA MAGHARIBI

Tangu karne ya IV umonaki ulienea Magharibi pia: zinajulikana monasteri za kike na za kiume huko Italia, Ufaransa na Hispania.

Babu bora wa Kanisa lote, mt. Augustino (350-430), baada ya kuongoka na kuzitembelea baadhi, alirudi kwao aanzishe maisha ya pamoja Afrika Kaskazini pia. Kwanza aliishi na walei wenzake, halafu alipochaguliwa kuwa askofu aliishi na mapadri wake, akiwashirikisha utajiri wake wa akili na roho, wafanye vizuri utume. Katika kanuni yake, iliyowalenga wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe la utawa, si jambo mojawapo tu.

Mt. Benedikto wa Nursia (480-547), ingawa si mwanzilishi wa umonaki wa Magharibi, ndiye aliyeuunda kwa namna ya kudumu na kwa njia hiyo akaja kuunda upya Ulaya Magharibi. Hasa kanuni aliyoitunga polepole, kutokana na mang’amuzi yake na mafundisho ya Bazili na ya mababu wa jangwani, iliunganisha vizuri maelekeo mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi upwekeni na kuishi kwa umoja. Sifa nyingine ni mchanganuo mzuri wa sala na kazi mbalimbali ambazo zilirekebisha na kufufua uchumi wa Ulaya na kuokoa elimu ya zamani. Yeye alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana abati ana nafasi ya pekee kama baba na mwalimu wa kudumu wa wamonaki wote, ambao wanafafanuliwa na Kanuni kuwa ndio “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati mmoja”. Kwake monasteri ni shule ya utumishi wa Bwana, ambapo abati ndiye mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo za misusuko (baada ya mfululizo wa uvamizi wa makabila ya Kijerumani), Benedikto alidai udumifu katika monasteri. Kutokana na kujitegemea kwa kila monasteri, Wabenedikto wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na kanuni. Ushirikiano kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na mitindo yake.

Kati ya mitindo mingine ya umonaki wa Magharibi ambayo ikaja kukubali kanuni ya Benedikto inakumbukwa hasa ile ya Wakristo wa Kiselti (Ireland n.k.) ambao hawakuwa na majimbo bali walimtegemea askofu-abati wa monasteri ya jirani na kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya mara kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa mt. Kolumbani (540-615).

Hata Wabenedikto walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf. mt. Augustino wa Canterbury (+604), mtume wa Uingereza, na mt. Bonifas (672-754), shahidi mtume wa Ujerumani.



MAREKEBISHO YA KARNE YA X-XII

Ni kawaida ya binadamu kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kulegea, kuanza safari kwa kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi tofauti za bidii na za ulegevu. Kanisa lenyewe, ingawa ni takatifu, linapatwa na ulegevu na ukosefu wa wanae. Ila Roho Mtakatifu haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili kulirekebisha. Utawa wenyewe ulianzishwa jangwani ili kupinga ulegevu wa Kanisa na unahusika kabisa na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili pia.

Hasa katika karne ya X-XII Kanisa la Magharibi lilitambua wazi haja ya urekebisho katika umonaki na katika maisha yake yote. Kati ya matawi mapya ya Kibenedikto yaliyotokana na juhudi hizo yanakumbukwa hasa lile la Cluny (lililokazia liturujia kuliko kazi za mikono), lile la Citeaux (ambalo lilirudia maisha magumu katika ufukara na kazi, likamtoa mt. Bernardo – 1091-1153 - aliyeathiri nyakati zake na zile zilizofuata, hasa upande wa maisha ya Kiroho), lile la Camaldoli (lililofufua ukaapweke) na mengineyo.

Wakati huohuo mt. Bruno (1035-1101) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na juhudi hadi leo (Wakartusi).



UKANONI KWA UREKEBISHO WA MAKLERI

Ili kurekebisha maisha ya mapadri, toka zamani ulisisitizwa uundaji wa jumuia kati yao, ambamo waishi na kusali na kufanya utume kwa pamoja. Hasa karne za XI-XII wengi walifanya hivyo kwenye makanisa makuu au makubwa na kueneza mtindo mpya wa kitawa unaosisitiza liturujia ya fahari pamoja na uchungaji. Walifuata kanuni ya mt. Augustino na kuitwa Wakanoni. Hata wao walichangia ustawi wa Kiroho wa Kanisa. Mkuu katika ya watakatifu wao ni Norbert (1082-1134), mwanzilishi wa Wapremontree.



WATAWA ASKARI NA WA HOSPITALI

Katika karne ya XII Wakristo walianzisha vita vya msalaba dhidi ya Waislamu hasa katika nchi takatifu. Kwa ajili hiyo ilianzishwa aina mpya ya watawa ambao, pamoja na maisha ya Kiroho washike upanga ili kusindikiza, kulinda na kukaribisha waliohiji Yerusalemu. Baadhi ya mashirika hayo yanadumu mpaka leo, lakini yamebadili sana malengo na mbinu.



MASHIRIKA YA WAOMBAOMBA

Kama kawaida bidii kwa urekebisho wa Kanisa zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei hawakuridhika. Pia hija na vita vya Msalaba vilifanya wengi wajionee nchi ya Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake. Ndiyo sababu walistawisha mifumo mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya Kanisa la mwanzoni, wakisisitiza ufukara na unyofu dhidi ya mwenendo wa mapadri na wamonaki, hata wengi walifikia hatua ya kuliasi Kanisa. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu kadhaa waukinai. Juu ya misingi hiyo yalianzishwa mashirika mbalimbali yaliyoitwa ya waombaomba kwa jinsi walivyokaza ufukara.

Mt. mzee Dominiko (1170-1221) akiwa padri aliguswa na uenezi wa uzushi akajitahidi kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu wote kama mhubiri halisi wa Injili alishika ufukara wa Yesu na mitume wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya kuchukua chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya kazi ya kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa ajili hiyo utawa wake ulipunguza miundo ya monaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya kusoma na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia ukweli ambao wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha. Ndio utume unaolingana zaidi na maisha ya sala na kusoma.

Hata kuliko rafiki yake Dominiko, mt. mzee wetu Fransisko (1181-1226) alishikwa na hamu ya kulingana na Yesu kwa kufuata nyayo zake inavyofundishwa na Injili. Alifanya vilevile kazi ya kuhubiri, lakini si kwa kuzingatia elimu wala kwa lengo la kubishana na wazushi, bali kwa kuonyesha njia ya toba kwanza kwa matendo halafu kwa maneno machache na manyofu. Kwa ajili ya Kristo alijinyima hata upweke alioupendelea, akawakaribia watu hasa wadogo. Utawa wake hauhitaji monasteri wala maktaba kubwa. Jamaa inategemea ndugu wenyewe na nyumba yao ni ulimwengu wote, ni popote pale wanapokutana. Katika kuzungukazunguka au walau kuhamahama, ndugu wadogo walilingana na watu wa zamani hizo: hawakujifunga kuishi daima mahali fulani na watu walewale, bali walifungamana na jamaa ya kimataifa ambayo mkuu wake aweze kuwatuma popote. Hivyo iliwabidi kuwa tayari kukabili mazingira yoyote na kushirikiana na ndugu mbalimbali. Tena udugu haukuishia shirikani bali ulitakiwa kuenea kwa watu na viumbe vyote. Kutokana na upya wa mtindo wa maisha, hata miundo ya utawa ilipaswa kuwa mipya ili kudumisha umoja wao. Ufransisko ulilingana kikamilifu na madai ya urekebisho ya walei, pia uliwapendeza viongozi wa Kanisa walioona ulivyookoa utiifu wa watu kwao: hivyo ulienea kasi ajabu, hata kati ya wanawake na watu wa ndoa. Watawa wa kike hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa ndugu wadogo. Mt. Klara (1193-1253), mche mdogo wa mt. Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza kutunga kanuni ya kitawa.



MASHIRIKA YA KUTOA HUDUMA

Hata karne ya XVI ilidai sana urekebisho wa Kanisa lote. Katika jitihada hizo wengine walifikia hatua ya kujitenga (Uprotestanti), wengine walianzisha matapo mapya ya Kiroho na mashirika ya aina mpya, yanayolenga hasa utume, kwa kupunguza ukubwa wa nyumba na liturujia ya pamoja: pengine jumuia ni kuishi mahali pamoja bila ya ushirikiano isipokuwa kati ya kiongozi na mtawa mmojammoja. Mashirika hayo hayana kanuni isipokuwa katiba tu.

Kati ya yote lile la Yesu (Wajesuiti) ndio muhimu zaidi. Mwanzilishi wake ni mt. Ignas wa Loyola (1491-1556) ambaye kabla hajaongoka alikuwa askari, halafu akaleta utawani mtindo wa kijeshi, akisisitiza utiifu kwa viongozi wa shirika na kwa papa (wakijifunga kwake kwa nadhiri ya nne, nguzo kuu ya shirika). Hivyo Mjesuiti jumuia yake halisi ni shirika tu ambalo linaweza kumtuma popote duniani na kumbadilishia kazi yoyote, naye atafanya yote kwa niaba ya shirika, tayari kukabili mazingira na hali yoyote.

Zaidi ya mashirika 2000 yaliyoanzishwa baada ya hapo, hasa katika karne ya XIX, yalifuata kwa kiasi fulani mtindo huo, yakilenga hasa huduma fulani iliyoonekana inahitajika lakini haina wa kuitoa, k.mf. kuhubiri vijijini, kulea vijana, kufundisha fukara, kuuguza wagonjwa, kuanzisha misheni, kushughulikia upashanaji habari. Mara nyingi mashirika hayo yanafanana ingawa yalianzishwa wakati tofauti na mahali tofauti, kwa kawaida chini ya askofu wa jimbo. Polepole hata wanawake walikubaliwa kufanya utume na kuanzisha mashirika ya namna hiyo.



MASHIRIKA YASIYO YA WAKFU

Karne hizohizo zilijitokeza pia aina nyingine ambazo pengine hazina nadhiri au si za hadhara. Kati ya wanawake mt. Anjela Merici (1474-1540) alianzisha muundo kwa wasichana kulelewa nyumbani ili kujitolea kutenda huruma. Vilevile walifanya Mary Ward (1585-1645) na mt. Luisa wa Marillac (1591-1660), wakitaka wafuasi wao waishi na kutumikia kati ya watu. Upande wa wanaume tunamkumbuka hasa mt. Filipo Neri (1515-1595) kati ya walioanzisha jumuia za maisha ya kitume ambapo watu wanaishi pamoja ili kujipatia malezi na kufanya utume fulani, lakini bila ya kujiweka wakfu.



KARNE YA XX

Karne hiyo ngumu kwa Kanisa na kwa dunia yote ilipata mang’amuzi mapya hasa katika maisha ya ulimwenguni. Kwa mara nyingine walei walichangia sana hali mpya ndani ya Kanisa, ya kuthamini na kushughulikia mambo ya kidunia. Katika juhudi za kuratibu nyanja zote za maisha ya binadamu, baadhi walijisikia haja ya kujiweka wakfu bila ya kujitenga na maisha ya kawaida. Polepole Kanisa likawakubalia (1950) wito mpya wa mashirika ya ulimwenguni ambayo waamini wanawekwa wakfu wawe chumvi, mwanga na chachu kati ya watu. Hivyo wanajitahidi kuwa na moyo wa kujikana na bidii ya kitume kama watawa, lakini pia utaalamu wa kisasa na urahisi wa kupenya mazingira yoyote kama walei.

Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikano (1962-1965) uliagiza uanzishwe tena utawa wa mabikira ambao waishi ulimwenguni na kuwekwa wakfu kwa ajili ya jimbo, si kwa shirika lolote.

Upande mwingine watu wa karne hiyo waliona haja ya kujumuika hata nje ya miundo ya kitawa, wakifuata mitindo wa kimonaki au kutoa huduma kwa wasiojiweza ndani ya jumuia, ingawa baadhi yao wana ndoa au pengine si Wakristo.

Nusu ya pili ya karne hiyo ilililetea Kanisa neema za matapo mengi yaliyoanzishwa kwa kawaida na walei na kuenea kati ya watu milioni na milioni. Mbali ya watawa wengi kuyafuata, na miito mingi kupatikana ndani yake, pia baadhi ya wafuasi wa matapo hayo hawaingii katika shirika fulani bali wanakusanyika kuishi kijumuia au kuwekwa wakfu katika matapo yenyewe na hivyo kuyaongoza Kiroho kwa kuchimba karama yake.

Muundo wa pekee ulikubaliwa kwa Opus Dei ambayo ina askofu wa pekee pamoja na mapadri wake, seminari mbalimbali na walei popote duniani: ni kama jimbo lisilo na eneo maalumu.

Mbele ya upya huo wote sheria za Kanisa siku hizi zinamhimiza askofu yeyote atambue aina mpya za maisha yaliyowekwa wakfu zikijitokeza jimboni.

Kazi nyingine ya Roho Mtakatifu ni kuanzishwa upya kwa mashirika ya kitawa katika Uprotestanti baada ya huo kuyafuta karne ya XVI kama kitu kinyume cha Injili. Kuanzia mwaka 1836 katika nchi mbalimbali watu wa madhehebu hayo walianza tena kuishi kijumuia kwa kufuata mapokeo ya Kibenedikto na ya Kifransisko.